• Machar apuuza makataa ya masaa 48 ya Kiir kumtaka arejee Juba

Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amekataa kuheshimu makataa ya masaa 48 aliyopewa na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo awe amerejea katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.

James Gatdet Dak, msemaji wa Machar amesema makamu huyo wa rais hatorejea Juba hadi pale kikosi cha tatu cha jumuiya ya kieneo ya IGAD kitakapotumwa nchini humo kudhibiti hali.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

 

Siku ya Alkhamisi, Rais Salva Kiir alimpa makamu wake masaa 48 awe amerejea mjini Juba kwa kile alichosema kuwa, kuendeleza utekelezaji wa makubaliano ya amani. Kadhalika Rais Salva Kiir aliahidi kudhamini usalama wa Machar wakati wa kurejea kwake mjini Juba. Machar alitoweka mjini Juba tangu yaliposhadidi mapigano kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono na wale wa Rais Kiir mjini hapo.

Riek Machar, makamu wa Rais wa Sudan Kusini

Ezekiel Lol Gatkuoth, mwanadiplomasia na mpambe wa Machar pamoja na wafuasi wengine wa mrengo wa Machar wakiwemo Alfred Lado Gore na Jenerali Taban Deng Gai walitoa taarifa ya pamoja na wafuasi wa Kiir, kupinga pendekezo la kutumwa vikosi vya kigeni nchini humo.

Watu wanakimbia machafuko mjini Juba, Sudan Kusini

Machafuko mapya mjini Juba yaliibuka tarehe saba mwezi huu ambapo hadi sasa watu zaidi ya 300 wameripotiwa kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine wamelazikika kukimbia nchi. Kadhalika machafuko hayo yameathiri makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana 2015 kati ya mahasimu hao wawili.

Jul 23, 2016 04:09 UTC
Maoni