Dec 16, 2016 08:18 UTC
  • Faili la jinai dhidi ya binadamu nchini Gabon latumwa ICC

Mawakili wa Jean Ping, kiongozi wa upinzani na mgombea wa kiti cha urais nchini Gabon aliyeshindwa na Rais Ali Bongo katika uchaguzi wa mwezi Agosti mwaka huu wametuma faili la jinai dhidi ya binadamu nchini humo, katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Mawakili hao wanaituhumu serikali ya Rais Ali Bongo kuwa imekiuka haki za binadamu na kutenda jinai kubwa dhidi ya binadamu, kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo baada ya uchaguzi wa rais wa mwezi Agosti.

Jean Ping, mkuu wa upinzani Gabon

Wapinzani nchini humo wanasema watu 26 waliuawa katika machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyoanza Agosti 31, huku takwimu rasmi za serikali zikisema ni watu watatu pekee waliuawa katika ghasia hizo.

Mkuu wa mawakili hao Emmanuel Altit raia wa Ufaransa amesema kufuatia uchunguzi wao wa kina ndani ya miezi mitatu iliyopita, vyombo vya usalama nchini Gabon vilitenda jinai dhidi ya binadamu na haswa hujuma dhidi ya raia wasio na hatia mjini Libreville Agosti 31 ambapo watu kadhaa waliuawa, kwa shabaha ya kung'ang'ania madaraka.

Hata hivyo serikali ya Gabon ilimuandikia barua Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, iliyodai kuwa kinara wa upinzani nchini humo na wafuasi wake ndio wanaochochewa wananchi kufanya mauaji ya kimbara na za kibinadamu.

Rais Ali Bongo wa Gabon

Matokeo ya uchaguzi huo yaliyolalamikiwa ndani na nje ya Gabon yalionyesha kwamba, Rais Ali Bongo alishinda kwa kupata asilimia 49.85 huku mpinzani wake mkuu Jean Ping akipata asilimia 48.23 ya kura. 

 

Tags

Maoni