Apr 11, 2017 16:35 UTC
  • Watu 16 wauwa katika mapigano nchini Sudan Kusini

Kwa akali watu 16 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi nchini Sudan Kusini.

Taarifa ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS imesema kuwa, makabiliano hayo yametokea katika mji wa Wau ambao ni wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Taarifa ya UNMISS imeongeza kuwa, haya ni makabiliano makali ya pili kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni nchini humo, haswa kuzingatia kuwa mapigano mengine kati ya askari wa serikali ya Juba na magenge ya waasi yalishuhidiwa hivi karibuni katika mji wa Pajok.

Mkazi wa mji wa Wau kwa jina Tibur Erynio ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, waliouawa katika makabiliano hayo ni watu 18, aghalabu yao wanaotoka katika makabila ya watu wachache ya Jur na Balanda.

Mauaji ya raia wasio na hatia katika mji wa Wau

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema watu zaidi ya 6,000 wamekimbilia kaskazini mwa Uganda kujisalimisha na mauaji ya raia yanayofanywa na askari wa serikali katika mji wa Pajok.

Hata hivyo, Kanali Santo Domic Chol, Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini amekanusha madai kuwa askari wa nchi hiyo wamewashambulia raia katika miji hiyo miwili akisisitiza kuwa wao wamekuwa wakipambana na waasi tu. 

Tags

Maoni