• Kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu nchini Nigeria

Baada ya viongozi wa Nigeria kukataa kumuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Waislamu wa nchi hiyo kwa mara nyingine tena wameandamana wakitaka kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu.

Mbali na jimbo la Kaduna, maandamano mengine kama hayo yamefanyika katika miji kadhaa ya Nigeria ukiwemo wa Katsina, Bauchi, Gombe na Minna. Maandamano hayo ya amani yaliingiliwa na polisi ambao waliwafyatulia risasi waandamanaji.  Vyombo vya usalama vya Nigeria vikiwa na lengo la kusambaratisha maandamano hayo viliwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji. 

Viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wanasema kuwa, vitendo hivyo vya utumiaji mabavu vilivyofanywa na polisi huko Kaduna dhidi ya Waislamu havikubaliki hata kidogo. Aidha viongozi hao wanasema kuwa, katika kipindi cha miezi kadhaa nyuma polisi imekuwa ikitoa mafunzo kwa magenge ya wahalifu ili yawashambulie wafuasi wa harakati hiyo ya Kiislamu. Hii si mara ya kwanza kwa maandamano ya amani ya Waislamu wa Nigeria wanaotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky kuingiliwa na polisi na kugeuzwa kuwa uwanja wa utumiaji mabavu dhidi ya raia.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria

Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni yeye pamoja na mkewe Disemba 2015 wakati jeshi lilipovamia na kushambulia mkusanyiko wa amani wa kidini wa wanachama wa IMN katika mji wa Zaria kaskazini mwa Nigeria ambapo mamia ya wanachama wa harakati hiyo ya Kiislamu waliuawa shahidi wakiwemo watoto wa Sheikh Zakzaky.

Tangu wakati huo, Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakishikiliwa kizuizini na vyombo vya usalama vya Nigeria. Licha ya kupita miezi kadhaa tangu Mahakama ya Federali ya nchi hiyo iagize kuachiwa huru Sheikh Zakzaky kutokana na kutokuwa na hatia, lakini serikali ya nchi hiyo imekataa kutekeleza takwa hilo la mahakama. Tangu Sheikh Zakzaky atiwe mbaroni, Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya maandamano kila leo wakitaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo.

Pamoja na hayo yote, ni muda sasa ambapo jeshi la Nigeria limeongeza mashinikizo yake dhidi ya Waislamu. Kushambulia mikusanyiko ya Waislamu na kutumia nyenzo ya vitisho na utumiaji mabavu ni miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikitumiwa kama wenzo wa kukabiliana na Waislamu wa nchi hiyo. 

Waisalmu wa Nigeria wakiandamana ili kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky

Muhula wa kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky ulimalizika Januari 16 mwaka huu. Kwa muktadha huo kutoachiliwa huru Sheikh Zakzaky ni kinyume kabisa na sheria na ni jambo linalokinzana wazi na Katiba ya nchi hiyo. Viongozi wa Nigeria si tu kwamba, hawajachukua hatua yoyote ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, bali wameshadidisha mashinikizo yao dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo, kwa miongo mingi Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakiishi kwa amani na usalama na wenzao Wakristo.

Katika miaka ya hivi karibuni kufuatia kuibuka matukio mbalimbali barani Afrika na kushindwa siasa za kupenda makuu za baadhi ya tawala kama Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel ni mambo ambayo yamezifanya tawala hizo zilizingatie bara la Afrika na kufanya harakati za kuwa na satwa na ushawishi barani humo. Katika kutekeleza siasa hizo, kuwashinikiza Waislamu na kukuza hitilafu za kidini na kikaumu kwa upande mmoja na kutoa himaya na uungaji mkono wa kifedha kwa majeshi ya nchi husika kwa upande mwingine, ni mambo ambayo yamefanywa kuwa sera na mipango ya tawala hizo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky alipojeruhiwa vibaya Disemba 2015

Nigeria inakabiliwa na mivutano hiyo katika hali ambayo, hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo hairidhishi. Harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo zinaendelea kushuhudiwa. Fauka ya hayo, kwa sasa Nigeria inakabiliwa na ukame na uhaba wa chakula hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo na hivyo kutishia uhai wa raia wengi wa maeneo hayo. Si hayo tu, kuzorota uchumi wa Nigeria kufuatia kupungua bei ya mafuta katika soko la dunia, kutofanikiwa kuwavutia wawekezaji wa kigeni, kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira ni matatizo mengine yanayoikabili nchi hiyo.

Katika mazingira kama haya, kuendelea kumshikilia korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky na kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria, hakutakuwa na matokeo mengine bighairi ya kuzidi kuufanya mgogoro wa nchi hiyo uongezeke na kuchukua mkondo mpana zaidi.

 

Apr 19, 2017 12:11 UTC
Maoni