• Hofu yatanda baada ya maafisa wawili kuuawa katika soko la Kinshasa

Hofu imetanda katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa baada ya watu wasiojulikana kuvamia soko kuu mjini humo na kuua maafisa wawili wa ngazi za juu.

Msemaji wa Polisi Pierrot Mwanamputu amethibitisha kuwa naibu kamanda wa polisi na msimamizi wa soko hilo waliuawa Ijumaa baada ya  kushambuliwa na watu wasiojulikana ambao pia waliwafungulia wafungwa. Aidha amesema maofisa wa polisi sita wamejeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali. Pia vituo viwili vya polisi katika eneo la soko vimeteketezwa.

Washambuliaji hao walishambulia ofisi ya msimamizi wa soko na kituo cha polisi sokoni na kuruhusu wafungwa waliokuwa wanashikiliwa gerezani kukimbia.

Wauzaji katika soko hilo wanasema hofu imetanda katika eneo hilo kwa sababu ofisi ya msimamizi ilishambuliwa pamoja na seli za polisi ambapo wafungwa wameachiliwa huru.

Maandamano ya wapinzani Kinshasa

Hakuna kundi lililodai kuhusika na tukio hilo lakini baadhi ya duru zinadokeza kuwa, hujuma hiyo ilitekelezwa na wanamgambo wa Bundi dia Kongo wanaopigana kujitenga na ambao walidaiwa kuhusika na hujuma ya gereza kuu Kinshasa mwezi Mei ambapo wafungwa 4,000 walitoroka.

Hali ni tete nchini DRC baada ya wapinzani kumtuhumu Rais Joseph Kabila, aliyeingia madarakani mwaka 2001, kuwa anachelewesha kwa makusudi uchaguzi wa rais ili aendelee kubakia madarakani hata baada ya muhula wake wa utawala kumalizika mwezi Disemba mwaka jana. Lakini Kabila anasema sababu ya kucheleweshwa uchaguzi ni ukosefu wa pesa na kutomalizika kwa wakati zoezi la kuandikisha wapiga kura.

Jul 16, 2017 06:51 UTC
Maoni