• Wanajeshi watatu wauawa katika uasi jeshini Ivory Coast

Wanajeshi watatu wameuawa katika uasi mpya ulioibuka katika jeshi la Ivory Coast.

Taarifa zinasema wanajeshi hao walipoteza maisha katika ufatulianaji risasi ulioibuka katika kituo cha kijeshi cha Korhogo kaskazini mwa Kodivaa.

Wakaazi wa Abdijan mji mkuu wa kibiashara wa Kodivaa wameripoti pia kusikia milio ya risasi karibu na kituo cha zamani cha askari wa umoja wa mataifa Jumamosi alfajiri.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa uasi wa wanajeshi nchini Ivory Coast. Malalamiko ya uasi ya wanajeshi hao ambao wengi wao katika mji wa Bouake walimsaidia Rais Ouattara kuingia madarakani yalianzia katika mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo na kuenea hadi Abidjan na miji mingine.

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast

Mwezi Januari mwaka huu kulishuhudiwa uasi kama huo, hata hivyo ulifikia tamati baada ya mazungumzo ya maafisa wa ngazi za juu na wanajeshi hao waasi na ahadi za Rais Alassane Ouattara za kulipwa marupurupu wanajeshi hao, kupatiwa nyumba na kuongezewa mshahara. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uasi wa mara hii wa wanajeshi ni wa kulalamikia kutotekelezwa ahadi zilizotolewa na Rais Alassane Ouattara.

Licha ya kuwa wanajeshi waasi wametangaza wazi kwamba, wako pamoja na Rais Alassane Ouattara na wanachodai wao ni kuboreshwa tu hali yao, lakini mvutano wa sasa umeongeza wasiwasi wa kutokea mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Jul 16, 2017 06:55 UTC
Maoni