• Edward Ngoyai Lowassa
    Edward Ngoyai Lowassa

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika Agosti 8 mwezi ujao.

Msimamo huo umetangazwa na Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia aligombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi uliopita wakati alipofanyiwa mahojiano maalumu na kusisitiza kuwa, Uhuru Kenyatta ni chaguo bora la demokrasia nchini Kenya.

Lowassa ambaye alikuwa Kenya kushiriki mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Joseph Ole Nkaissery amemtaja Uhuru Kenyatta kama mtu mzurim anayeunga utangamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambaye anawawaheshimu viongozi wa upinzani.

Edward Lowassa akifanyiwa mahojiano jijini Nairobi

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, chama cha upinzani cha Chadema kinamuunga mkono Rais Kenyatta, kutokana na uhusiano wa karibu ulipo kati ya Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Taifa wa Chadema alinukuliwa mwezi Mei mwaka huu akimtaja Raila Odinga kuwa ni msaliti kutokana na kumuunga mkono Rias Magufuli.

Mbowe alinukukuliwa akisema kuwa, katika uchaguzi wa mwaka 2013 nchini Kenya, tulimuunga mkono Raila Odinga, lakini tulishangazwa mno katika uchaguzi wa mwaka 2015 nchini Tanzania wakati Odinga alipotangaza kumuunga mkono mgombea uraia kwa tiketi ya CCM John Pombe Magufuli.

 

Jul 16, 2017 15:20 UTC
Maoni