• Zaidi ya watu 30  hawajulikani waliko nchini Cameroon baada ya boti yao kuzama

Zaidi ya watu 30 wamepotea nchini Cameroon na hadi sasa hawajulikani waliko siku moja baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Cameroon imeeleza kuwa, boti hiyo iliyokuwa na abiria 37 wakiwemo wanajeshi ilizama wakati ilipokuwa ikielekea katika mji wa Bakassi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo wanajeshi watatu wameokolewa huku abiria 34 wa boti hiyo wakiwa bado hawajapatikana hadi sasa.

Uchunguzi na juhudi za kuwatafuta wahanga wa ajali hiyo zinaendelea huku timu maalumu ya uokozi ikiwa imetumwa katika pwani ya Cameroon.

Wizara ya ulinzi nchini Cameroon imesema boti hiyo ilipoteza mawasiliano kuanzia mapema wakati ikitokea jijini Duala ikielekea Bakasi saa moja kabla ya kupoteza mawasiliano.

Wapiganaji wa Boko Haram

Jeshi la Cameroon linaunda kikosi cha kieneo cha nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika kinachoendesha mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo wa Boko Haram ambao wamehatarisha maisha ya watu nchini Nigeria na maeneo ya jirani na nchi hiyo.

Watu zaidi ya 20,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2.5 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria tangu kundi la Boko Haram lianzishe hujuma zake nchini Nigeria mwaka 2009.

Serikali ya Rais Muhammadu Buhari imekuwa ikilaumiwa kutokana na kushindwa kukabiliana na wanamgambo hao ambao wamekuwa wakitenda jinai za kutisha.

Jul 17, 2017 13:58 UTC
Maoni