• Serikali ya Kongo DR yataka kutangazwa hali ya hatari nchini humo

Kufuatia mapigano yaliyojiri mjini Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, vyama viwili vya kisiasa washirika vinavyounda serikali ya nchi hiyo, vimetaka kutangazwa hali ya hatari nchini.

Baada ya kujiri mapigano makali siku ya Ijumaa katika soko la mjini Kinshasa, chama cha (PRPD) na chama tawala nchini humo vimetoa taarifa ya pamoja ya kutaka kutangazwa kwa hali ya hatari nchini kwa kutegemea kipengee cha 144 cha katiba. Katika ripoti hiyo, vyama hivyo vimesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inahitaji mshikamano kwa ajili ya kupambana na kile kilichotajwa kuwa ni ugaidi.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Wakati huo huo, wapinzani wa serikali wamepinga na kukosoa suala hilo na kusema kuwa, kutangazwa hali ya hatari kuna maana ya kuzuiwa uhuru sambamba na kutoa mwanya wa kuahirishwa tarehe ya uchaguzi mkuu nchini. Hii ni katika hali ambayo Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo imetangaza hivi karibuni juu ya kuwepo uwezekano wa kuahirishwa kwa tarehe ya uchaguzi mkuu nchini humo. Christophe Lutundula, mmoja wa wanasiasa wa upinzani na mjumbe wa kundi la vyama saba vya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (G7) sambamba na kutangaza upinzani wake juu ya pendekezo hilo la serikali kwa ajili ya kuahirishwa uchaguzi mkuu, amesema kuwa uahirishwaji huo unapangwa  kwa lengo la kutaka kumbakisha madarakani zaidi Rais Joseph Kabila.

Sehemu ya makundi ya waasi wa nchi hiyo

Amesema kuwa, kuahirishwa uchaguzi, ni kinyume na katiba na hata makubaliano ya tarehe 31 Disemba mwaka jana 2016 yaliyofikiwa kati ya serikali na vyama vya upinzani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo Rais Joseph Kabila anatakiwa kuondoka madarakani ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

 

 

Jul 17, 2017 14:07 UTC
Maoni