Aug 07, 2017 16:33 UTC
  • Jeshi la Sudan Kusini lateka ngome kuu ya waasi ya Pagak

Jeshi la serikali ya Sudan Kusini limefanikiwa kutwaa ngome kikuu ya waasi katika eneo la Pagak lililoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia.

Mapigano ya kutekwa eneo hilo yamewalazimisha maelfu ya wakazi wa mji huo kukimbia nyumba na makazi yao. Eneo hilo limekuwa likidhibitiwa na waasi wa Sudan Kusini tangu mwaka 2014.

Msemaji wa waasi, Lam Paul Gabriel amesema kuwa, wamelazimika kuondoka katika eneo la Pagak kutokana na mashambulizi makali ya jeshi la serikali mapema jana Jumapili.

Eneo la Pagak ambalo liko katikati ya makazi ya watu wa kabila la Nuer, limekuwa kituo kikuu cha operesheni za waasi wa Sudan Kusini tangu mwaka 2014. 

Waasi wa Sudan Kusini

Msemaji wa waasi, Lam Paul Gabriel amesema kuwa, kutwaliwa kwa eneo la Pagak hakuna maana ya kukomeshwa mapambano ya watu wa kabila la Nuer dhidi ya serikali inayodhibitiwa na watu wa kabila la Dinka ya Sudan Kusini.

Nchi hiyo ilitumbukia kwenye vita na mapigano ya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar wa kabila la Nuer kuwa alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. 

Tags

Maoni