• Watu 11 wauawa katika machafuko Kenya; maandamano ya kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta yaendelea

Watu 11 wanaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi nchini Kenya katika mandamano na vurugu za kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta aliyetangazwa jana na Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo IEBC kuwa ndiye mshindi wa kiti cha Urais.

Maadamano hayo yaliyoanza jana katika miji ambayo ni ngome za kiongozi wa upinzani Raila Odinga hasa mjini Kisumu na ambayo yameendelea hadi leo, yamezua wasiwasi mkubwa huku washiriki wa maandamano hayo wakisisitiza kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, hali ya wasiwasi inaendelea kushuhudiwa katika mitaa kadhaa ya jiji la Nairobi na Kisumu nchini Kenya baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa Uchaguzi wa urais Ijumaa usiku.

Mjini Kisumu Magharibi mwa nchi hiyo, ambayo pia ni ngome kuu ya Raila Odinga, wafuasi wake wameendelea kuandamana kupinga ushindi wa Rais Kenyatta.

Wafuasi wa Odinga walioonekana wenye hasira, wamenukuliwa wakisema kuwa, hawayakubali matokeo hayo.

Polisi wakimpa kichapo mmoja wa waandamanaji

Hayo yanajiri huku kukiwa na taarifa kwamba, polisi imekuwa ikitumia risasi hai kukabiliana na waandamanaji hao.

Hata hivyo, taarifa hizo zimekanushwa vikali na Fred Matiang'i, Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya ambaye amesisitiza kuwa, polisi haijawafyatulia risasi hai waandamanaji.

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo, limelaani hatua ya Polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kuitaka kujiepusha kukabiliana na waandamanaji.

Aidha Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Huma Rights Watch limeitaka polisi ya Kenya kujizuia na kuacha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Aug 12, 2017 14:06 UTC
Maoni