• Upinzani Kenya: Jeshi la polisi limeua watu mia moja

Mrengo wa upinzani nchini Kenya umedai kwamba, jeshi la polisi nchini humo limeua watu mia moja tangu yalipoanza maandamano ya kulalamikia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Jumanne iliyopita.

Hata hivyo mrengo wa upinzani nchini Kenya haujatoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Madai hayo ya upinzani yanatolewa huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya kuripotiwa kwamba, watu 11 wameshauawa tangu Rais Kenyatta alipotangazwa siku ya Ijumaa kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamekitaka kikosi cha polisi nchini Kenya kuacha kutumia nguvu za ziada katika kukabiliana na maandamano ya wapinzani ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Hali si shwari katika baadhi ya maeneo ya Kenya

Upinzani unasisitiza kuwa, watu wasiopungua 100 wameuawa wikiwemo watoto kumi huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

James Orengo mmoja kati ya viongozi wa muungano wa upinzani wa NASA amesema kuwa, polisi wamekuwa wakichochea machafuko kutokana na ukandamizaji wanaoufanya dhidi ya waandamanaji.

Wakati huo huo, Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Fred Matiang'i amesema kuwa, polisi hawatasita kulinda maisha ya Wakenya na mali zao kufuatia kukamilika kwa uchaguzi uliokumbwa na utata.

Matokeo rasmi yaliyotangazwa yanaonyesha kuwa, Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote, huku mshindani wake mkuu Raila Odinga  aliyegombea kwa tiketi ya ODM akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote.

Aug 13, 2017 04:04 UTC
Maoni