• Makumi ya watu waaga dunia kwa kipindupindu DRC

Makumi ya raia wanaripotiwa kufariki dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na maradhi ya kipindupindu yaliyoibuka katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo imeelezea pia kuwa, hali ya kibinadamu katika maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni mbaya.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, licha ya hatua zilizochukuliwa za kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu tangu ulipoibuka nchini humo, lakini idadi ya wanaofariki dunia kwa ugonjwa huo imekuwa ikiongezeka kila siku. 

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa, hadi sasa zaidi ya watu 3,140 wanaugua kipindupindu katika mji wa Goma ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Daktari akikagua faili la mmoja wa wagonjwa wa kipindupindu katika moja ya vituo vya afya DRC

Aidha taarifa ya wizara hiyo ya afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeeleza kuwa, kasi ya kuenea maradhi ya kipindupindu iliongezeka baada ya kusimamishwa bila kutaka utekelezaji wa 'Mpango wa Usimamizi na Ugavi wa Maji DRC", suala ambalo lilisababishwa na kukatika kwa nishati ya umeme.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na maradhi ya kipindupindu mara kwa mara kutokana na kuwa na huduma duni za maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Ugonjwa wa kipindupindu ni miongoni mwa maradhi hatari na dalili zake kuu ni kuharisha, kutapika sana pamoja na homa kali.

 

Aug 13, 2017 13:43 UTC
Maoni