• Zambia kumuachia huru kiongozi wa upinzani, kumfutia mashtaka ya uhaini

Serikali ya Zambia inatazamiwa kumfutia mashitaka ya uhaini sambamba na kumuachia huru kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Hakainde Hichilema.

Duru za habari zimeliarifu shirika la habari la Reuters kuwa, Hichilema ataachiwa huru kesho Jumatatu, baada ya kuondolewa tuhuma za uhaini, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali, vyombo vya mahakama na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Hichilema ambaye ni mkuu wa chama cha UPND alikamatwa na vyombo vya usalama mapema mwezi Aprili mwaka huu, kwa tuhuma za kupanga njama ya kuipindua serikali. 

Rais Edgar Lungu wa Zambia

Vyombo vya usalama vilidai kuwa vimemtia nguvuni mwanasiasa huyo wa upinzani kwa kuzuia msafara wa magari ya Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo ya Kiafrika, magharibi mwa nchi. Serikali ya Zambia imekuwa ikikosolewa kwa kuwawekea mbinyo viongozi wa upinzani na wakosoaji wake.

Mapema mwezi huu, polisi ya Zambia ilimkamata kiongozi mwingine wa upinzani wa nchini humo, Saviour Chishimba kwa tuhuma ya kumtukana Rais Edgar Lungu, kosa ambalo adhabu yake inaweza kufikia kifungo cha miaka mitano jela.

Aug 13, 2017 14:01 UTC
Maoni