• Mgogoro nchini Kongo DR unawafanya watoto wengi zaidi walazimike kuacha masomo

Asasi moja isiyo ya kiserikali imetangaza kuwa watoto wengi zaidi wanakosa elimu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na mgogoro na mfumo duni wa elimu wa nchi hiyo.

Baraza la Wakimbizi la Norway limetoa ripoti na kueleza kwamba watoto wapatao 850,000 wamebaki bila makaazi na skuli 900 zimebomolewa kutokana na kushadidi machafuko katika mkoa wa Kasai katikati mwa Kongo DR katika kipindi cha mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa asasi hiyo idadi hiyo ya watoto ni sehemu ya watoto wapatao milioni saba na laki nne waliokosa masomo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku mgogoro huo ukisababisha idadi hiyo kuongezeka katika nchi hiyo yenye mfumo dhaifu wa elimu.

Makundi ya wanamgambo yanayopigana nchini Kongo DR

Ripoti ya Baraza la Wakimbizi la Norway imebainisha kuwa karibu asilimia 92 ya watoto wenye umri wa miaka sita hadi 11 wamekosa kwenda skuli katika miji iliyokumbwa na machafuko ya Kalemie na Tanganyika.

Asasi hiyo imetahadharisha pia kwamba nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika inakabiliwa na hatari ya kupoteza kizazi chake kijacho kwa sababu katika mwaka huu umetolewa mchango wa asilimia nne tu ya fedha za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya sekta ya elimu ya Kongo DR.

Baraza la Wakimbizi la Naorway limeongeza kuwa watoto waliotimiza umri wa kwenda shule wanachangia zaidi ya asilimia 17 ya watu wapatao milioni tatu na laki nane waliopoteza makaazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.../

Tags

Sep 12, 2017 07:52 UTC
Maoni