• Watu 25 Wauawa katika Mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati, Waziri wa Ulinzi afutwa kazi

Watu 25 wameuawa katika mapigano mapya huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) huku waziri wa ulinzi nchini humo akifutwa kazi kutokana na ongezeko la machafuko nchini humo.

Taarifa zinasema watu hao wameuawa katika mapigano yaliyojiri baina ya makundi ya wabeba silaha katika eneo la kati mwa nchi hiyo katika kipindi cha siku kadhaa zilizopita. Umoja wa Mataifa pia umetahadahrisha kuhusu wimbi jipya la mauaji nchini humo.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadera Jumanne usiku amemfuta kazi waziri wake wa ulinzi  Levy Yakete kutokana na ongezeko la mapigano yanayoendelea nchini humo.

Waziri huyo aliwahi kuwekwa katika orodha nyeusi ya kamati moja ya Umoja wa Mataifa mwaka 2014 kwa kuhusika katika mauaji dhidi ya Waislamu katika vita vya ndani nchini humo mwaka  2013.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé. 

Askari wa kulinda amani wa UN wameshindwa kuzuia mauaji CAR

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati  yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo,  François Bozizé. Baada ya rais Muislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Djotidia alilazimishwa na nchi za kieneo kujiuzulu mwezi Januari 2014 na hapo mauaji ya Waislamu yakashika kasi zaidi. Kabla ya kuanza mgogoro, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa na wakaazi 130,000 Waislamu lakini sasa taarifa zinasema idadi hiyo ni chini ya 1,000.

Aidha watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao huku wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wakiwa wanahitaji kusaidiwa. Mauaji ya Waislamu CAR yanajiri pamoja na kuwepo vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini humo.

Sep 13, 2017 07:39 UTC
Maoni