• Mwangwi wa hatua ya kinara wa chama kikuu cha upinzani Kenya kujiondoa katika uchaguzi wa Rais

Kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA) nchini Kenya ametangaza kuwa, hatagombea katika uchaguzi wa marudio wa rais ambao umepangwa kufanyika tarehe 26 Oktoba akisema kwamba uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki.

Raila Odinga amesema amejiondoa katika kinyang'anyiro hicho kwa maslahi ya watu wa Kenya, kanda ya mashariki mwa Afrika na duniani nzima. 

Amefafanua kuwa, muungano wa upinzani wa NASA umefikia hitimisho kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haina nia ya kuhakikisha ukiukaji wa taratibu na sheria za uchaguzi uliofanywa na tume hiyo katika uchaguzi uliopita hautokei tena.

Amebainisha kwamba ishara zote zilizopo zinaonyesha kuwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa mbovu zaidi kuliko uliotangulia.

Raila Odinga

Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa tarehe 8 Agosti ambayo yalionesha kuwa kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta alikuwa amemshinda mpinzani wake, kwa hoja kwamba, uchaguzi huo ulikiuka taratibu. Hatua hiyo ya Mahakama ya Juu ya Kenya ilikuwa na mwangwi mkubwa katika duru mbalimbali za kieneo na kimataifa na baadhi ya wachambuzi waliitambua kuwa ni matunda na mafanikio makubwa si kwa upinzani pekee bali kwa bara zima la Afrika na hatua muhimu katika utawala wa sheria na vilevile ishara ya kukomaa demokrasia barani Afrika. Katika uwanja huo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde aliitaja hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kuwa ni ishara ya kukomaa demokraia barani Afrika. 

Baada ya hapo Mahakama ya Juu ya Kenya ilitangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 26 mwezi huu wa Oktoba. Hata hivyo muungano wa upinzani wa NASA kilitangaza tangu awali kwamba, hakitashiriki katika uchaguzi huo iwapo masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa maafisa wa Kamisheni Huru ya Uchaguzi waliohusika katika dosari zilizopelekea kubatilishwa uchaguzi wa awali wa rais, hayatatekelezwa. Kwa hakika kambi ya upinzani ya Kenya ilitaka kufanyike mabadiliko ya kimsingi katika taasisi zinazosimamia uchaguzi ili kuhakikisha kwamba, chaguzi hizo zinafanyika kwa uhuru, uwazi na uadilifu. Hata hivyo masharti hayo hayakutekelezwa.

Machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 Kenya

Alaa kulli hal, uamuzi wa mgombea wa muungano wa upinzani wa kujiondoa katika uchaguzi wa marudio wa rais zikiwa zimebakia siku 16 tu kabla ya zoezi hilo, unaweza kuwa na taathira mbaya za kisiasa nchini Kenya na hata kusababisha ghasia na machafuko. Kwa msingi huo pande zote mbili za chama tawala cha Jubilee na muungano wa upinzani wa NASA zinapaswa kuwa na tahadhari na kuwa macho zaidi na kuhakikisha kwamba, Kenya haitumbukii tena katika machafuko kama yale ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Zaidi ya watu 1400 waliuawa katika machafuko hayo na maelfu ya wengine wakalazimika kuwa wakimbizi.  

Oct 11, 2017 10:54 UTC
Maoni