• Serikali ya Kenya yapiga marufuku maandamano ya upinzani katikati ya miji

Serikali ya Kenya imetangaza kupiga marufuku maandamano ya wafuasi wa muungano wa upinzani NASA katikati ya miji mikubwa nchini humo.

Serikali ya Kenya imesema kuwa, imepiga marufuku maandamano katika maeneo ya katikati mwa miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu. Kaimu Waziri wa Usalama  wa nchi hiyo Dakta Fred Matiang'i amesema pia kwamba wanaopanga maandamano wanafaa kuwajibishwa kutokana na uharibifu wa mali unaotokea wakati wa maandamano.

Hatua ya Dakta Matiang'i imetokea huku muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) wa  Raila Odinga ukiendelea na maandamano ya kushinikiza mageuzi katika Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Matiang'i ameongeza  kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya baadhi ya waandamanaji wa upinzani kupora mali ya watu katika miji hiyo siku ya Jumatano.

Mmoja wa viongozi wa Nasa James Orengo, ambaye alikuwa naibu ajenti mkuu wa Bw Odinga wakati wa uchaguzi wa mwezi Agosti ambao ulifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu, alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kuandamana kila siku.

Polisi ya Kenya ikitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji

Aidha, Waziri huyo amefafanua kuwa serikali haiwezi kuzuia maandamano kwa sababu ni haki ya Wakenya kama ilivyoanishwa kikatiba, kuandamana  ila inachofanya, ni kuepusha mali ya watu kuporwa na kuharibiwa.

“Tunafanya hivi ili kuzuia uharibifu wa mali ya watu na kuwalinda Wakenya wengine wasiotaka kuandamana,” alisema.

“Maandamano ni haki ya kila mtu kwa sababu hilo lipo kwenye Katiba ya nchi,” aliongeza Matiang'i.

Hata hivyo, waandalizi wa maandamano ya upinzani wakiongozwa na kiongozi wa vijana katika muungano huo Benson Musungu, wamepuuzilia mbali marufuku hayo na kusisitiza kuwa yataendelea kama ilivyopangwa siku ya Ijumaa. Musungu amesema maandamano ya Ijumaa yataendelea kama ilivyopangwa na kila siku kuanzia Jumatatu ijayo.

Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ambaye ametangaza kujiondoa kwenye Uchaguzi huo kwa kile alichosema kuwa, hajaridhishwa na maandalizi ya Tume ya Uchaguzi, yupo ziarani nchini Uingereza.

Tume ya Uchaguzi inasema, uchaguzi wa tarehe 26 utaendelea kama kawaida lakini wanasheria na wachambuzi wa siasa wanaotofautiana kuhusu uhalali wa Uchaguzi huo.

Oct 12, 2017 11:22 UTC
Maoni