• Jumuiya ya Waislamu wa jimbo la Ogun Nigeria yalalamikia marufuku ya hijabu mashuleni

Jumuiya ya Waislamu wa jimbo la Ogun la kusini magharibi mwa Nigeria wamelalamikia vikali marufuku ya hijabu mashuleni katika jimbo hilo na kuwataka viongozi wa jimbo hilo kuruhusu wanafunzi wasichana wa Kiislamu kuingia katika shule za mji huo wakiwa wamejisitiri kwa vazi hilo la Kiislamu.

Wakizungumza katika mkutano wao katika Msikiti wa Abeokuta katika jimbo la Ogun, viongozi hao wa Jumuiya ya Waislamu wamewataka viongozi wa serikali kuwaruhusu mabinti wa Kiislamu kuvaa hijabu sambamba na sare za shule.

Tajuddin Adiwunmi, Katibu Mkuu wa Muungano wa Viongozi wa Kidini Nigeria ametoa wito katika mkutano huo wa Jumuiya ya Waislamu kupambana na sheria zilizo dhidi ya Uislamu.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa, uhuru wa dini ni jambo ambalo limeheshimiwa na kubainishwa wazi na Katiba ya Nigeria na kwamba, vazi la hijabu ni miongoni mwa sheria za Kiislamu.

Aidha wazazi wa wanafunzi wa Kiislamu walioshiriki katika mkutano huo wameeleza kutoridhishwa kwao hata kidogo na sheria inayopiga marufuku vazi la hijabu katika skuli za Nigeria.

Wasichana wa Kiislamu katika moja ya shule za Nigeria

Kadhalika wazazi hao wamelalamikia vikali vitendo vya walimu na viongozi wa shule wanaowaudhi na kuwabughudhi mabinti wa Kiislamu wanaojisitiri kwa vazi tukufu la Kiislamu la hijabu. 

Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakilalamikia sheria za baadhi ya majimbo ya nchi hiyo za kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule binafsi hasa katika maeneo ambayo wakazi wake wengi ni Wakristo.

Ikumbukwe kuwa, mapema mwezi Februari mwaka huu, Mahakama ya Rufaa katika jimbo la Lagos nchini Nigeria ilitoa hukumu ya kubatilisha amri ya serikali ya jimbo hilo ya kupiga marufuku vazi la Hijabu kuvaliwa na wasichana Waislamu shuleni.

Oct 13, 2017 03:51 UTC
Maoni