• Waziri wa Ulinzi wa Somalia na Mkuu wa Majeshi wajiuzulu

Waziri wa Ulinzi wa Somalia na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo waliokuwa wakiongoza vita dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabab wamejiuzulu.

Abdurahman Omar Osman, Waziri wa Habari wa Somalia amewaambia waandishi wa habari kwamba, Abdirashid Abdullahi Mohamed, Waziri wa Ulinzi na Jenerali Mohamed Ahmed Jimale mkuu wa majeshi ya nchi hiyo jana walikabidhi barua zao za kujiuzulu katika kikao cha wiki cha Baraza la Mawaziri.

Waziri wa Habari wa Somalia amesema kuwa, viongozi hao wawili wameeleza kuwa, wamejiuzulu nyadhifa hizo kwa sababu zao binafsi.

Hata hivyo baadhi ya duru zinasema kuwa, Waziri wa Ulinzi wa Somalia na mkuu wa majeshi wa nchi hiyo wamejiuzulu baada ya kuzuka hitilafu kati yao na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya usalama likiwemo suala la udhaifu katika kukabiliana na kundi la kigaidi la al-Shabab.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Waziri wa Habari wa Somalia ametangaza kuwa, tayari Rais Mohamed Abdullahi Farmajo  wa nchi hiyo amemteua Jenerali Abdi Jama Hussein kuchukua nafasi ya Mkuu wa majeshi kufuatia kujiuzulu  Jenerali Mohamed Ahmed Jimale huku nafasi ya Waziri wa Ulinzi ikiwa bado iko wazi.

Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi likiwemo suala la ukame na njaa pamoja na ukosefu wa usalama kutokana na harakati za kundi la kitakfiri la al-Shabab.

Kundi hilo la kigaidi lenye uhusiano na mtandao wa al Qaeda linalenga kuiangusha serikali ya Somalia.

Oct 13, 2017 04:06 UTC
Maoni