• Chad yaondoa askari wa jeshi lake Niger katika vita dhidi ya Boko Haram

Chad imeondoa mamia ya askari wake katika nchi jirani ya Niger ambako walikuwa wakitoa msaada kwa vikosi vya nchi hiyo kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Hayo yamethibitishwa na duru za utoaji misaada ya kibinadamu na maafisa wa serikali ya Niger huku kukiwa hakuna maelezo au kauli yoyote iliyotolewa hadi sasa na maafisa wa kijeshi wa Chad.

Kuondolewa askari hao ambako kumefanyika ndani ya muda wa majuma mawili yaliyopita kunaweza kudhoofisha juhudi za kieneo za kuyatokomeza magaidi ya kundi hilo la kitakfiri, ambalo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa limeshaua zaidi ya watu 20,000 katika nchi za Nigeria, Chad, Cameroon na Niger tangu lilipoanzisha mashambulio yake mwaka 2009, mbali na wengine zaidi ya milioni mbili waliolazimika kuwa wakimbizi na kuligeuza eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kuwa moja ya sehemu zenye hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani kwa kuwafanya watu wasiopungua milioni 10 na laki saba wahitajie misaada ya haraka.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram

Wakaazi hasa wa eneo la Diffa nchini Niger wamesema kuondoka kwa askari wa Chad tayari kumeshaathiri usalama wa eneo hilo ambalo limekuwa likishuhudia wimbi la mashambulio ya magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram wanaoingia ndani ya ardhi ya Niger kutokea kwenye ngome yao kuu kaskazini mashariki mwa Nigeria.../

Oct 13, 2017 07:35 UTC
Maoni