Oct 15, 2017 16:30 UTC
  • Idadi ya wahanga wa miripuko ya Mogadishu Somalia yafikia 231, Iran yalaani + Picha

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Shirika la habari la Fars limemnukuu Bahram Qassemi, akisema leo kuwa, Tehran inalaani shambulizi hilo la kigaidi na iko pamoja na familia za wahanga wa shambulio hilo, kuomboleza maafa yaliyowafika.

Wakati huo huo polisi nchini Somalia wametangaza kuwa, idadi ya wahanga wa miripuko miwili ya mabomu iliyotokea jana katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu imeongezeka na kufikia watu 231.

Polisi na duru za hospitali za Somalia zimeviambia vyombo vya habari kwamba, hasara zilizosababishwa na miripuko hiyo ya jana Jumamosi ambayo ni mikubwa zaidi kuwahi kutokea mjini Mogadishu tangu genge la kigaidi la al Shabab lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2007 imeongezeka na kufikia watu 231.

Jana Polisi ya Somalia ilitangaza kuwa watu wapatao 40 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya lori lililotegwa bomu kuripuka katika eneo lenye msongamano wa watu katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu. Wengi wa waliouawa na kujeruhiwa katika mripuko huo ni raia wa kawaida.

Hadi hivi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo lakini kundi la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaeda limekuwa likihusika na utegaji mabomu na mashambulizi mengi ya kigaidi ya aina hiyo ndani ya Somalia na katika nchi jirani.

Sehemu ya maafa ya miripuko ya kigaidi nchini Somalia
Sehemu ya maafa ya miripuko ya kigaidi nchini Somalia

 

Maoni