• Askofu asilimu Kenya na wafuasi wake, ageuza kanisa lake kuwa msikiti

Askofu mmoja nchini Kenya amesilimu akiwa na wafuasi wake na kulibadilisha kanisa lake kuwa msikiti.

Kwa mujibu Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA),  Askofu Charles Okwany ambaye baada ya kuichagua dini ya Kiislamu kuwa mwongozo wake wa wokovu duniani na Akhera amechagua jina la Ismail Okwany. Amesema amesilimu baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu Uislamu. Amesema baada ya kusilimu, kanisa alilokuwa akihurbiri, lililoko katika eneo la Nyalgosi kaunti ya Homa Bay magharibi mwa Kenya, ambalo lilijulikana kwa jina la God’s Call Church of East Africa sasa limegeuzwa jina na kuwa Msikiti  wa Jamia wa Nyalgosi.

Katika mahojiano na Jarida la Nairobian, Ismail Okwany amesema, wakati alipokuwa muhubiri wa Kikristo alikuwa akisafiri katika miji mbalimbali ya Kenya na Tanzania hasa katika maeneo ya pwani na alipata fursa ya kufanya utafiti kuhusu maisha ya Waislamu. Ismail Okwany anaongeza kuwa aliweza kulinganisha Uislamu na Ukristo na akaamua kufuatia Uislamu.

Waislamu wakiwa kwenye ibada katika eneo ambalo lilikuwa zamani ni kanisa katika eneo la Nyalgosi, kaunti ya Homa Bay, magharibi mwa Kenya

Aidha anasema moja ya mambo yaliyokuwa yakimkera sana wakati akiwa muhubiri wa Ukristo ni tabia ya wanawake kuingia ndani ya kanisa wakiwa wamevaa sketi fupi katika hali ambayo wanawake Waislamu wanakuwa wamejisitiri kwa Hijabu wakati wa ibada msikitini na hata nje ya msikiti.  Okwany mwenye umri wa miaka 65 alisilimu tarehe 26 Septemba akiwa na wafuasi kadhaa wa kanisa lake na sasa wako mbioni kusajili rasmi msikiti wao.

Tags

Oct 16, 2017 02:33 UTC
Maoni