• Tahadhari kuhusu njama za utawala wa Kizyauni wa Israel kujipenyeza zaidi Afrika

Makundi ya kisiasa nchini Tunisia yametahadharisha kuhusu mikakati ya utawala wa Kizayuni wa Israel barani Afrika.

Jumuiya ya Ansar Felestin au Marafiki wa Palestina na asasi kadhaa zisizo za kiserikali nchini Tunsia zimeitisha kikao na kutahadharisha kuhusu njama zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel barani Afrika na kuzitaka nchi za Afrika zichukue hatua za kukabiliana na utawala huo ghasibu barani humo.

Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake wanajaribu kueneza ushawishi wao katika nchi mbali mbali za Afrika. Ili kufikia lengo hilo, katika miaka ya hivi karibuni, kumeshuhudiwa harakati maalumu za wakuu wa Israel barani Afrika.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amezitembelea nchi kadhaa za Afrika na pia amekuwa akijaribu kuandaa bila mafanikio kikao cha Israel na Afrika.

Utawala wa Tel Aviv unaendeleza harakati za kujipenyeza Afrika kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kijeshi.

Katika uga wa kisiasa, utawala wa Kizayuni unatekeleza mkakati wa kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingi zaidi za Afrika na kuzitumia baadhi ya nchi hizo kuupigia kura utawala huo katika vikao vya kimataifa.

Netanyahu na Rais Museveni wa Uganda

Katika upande mwingine kutokana na kuendelea kupoteza itibari kimataifa utawala wa Kizayuni wa Israel, kufuatia jinai na ukatili wake dhidi ya Wapalestina, utawala huo sasa unalenga kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ili kujikwamua kutoka katika mgogoro wa kukosa uhalali. Israel inalenga kutumia nchi za Afrika ili kuzuia Wapalestina kufikia malengo ya ukombozi wao katika hali ambayo kwa miongo kadhaa nchi za Afrika zimekuwa mstari wa mbele kutetea Wapalestina.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, pia kwa kuzingatia kuwa bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa madini na mali asili pamoja na ustawi mkubwa wa kiuchumi wa bara hilo, utawala wa Israel unalitazama bara hilo kwa jicho la tamaa.  Hivi sasa kuna mashirika mengi ya Israel yanayoshiriki katika miradi mbali mbali barani Afrika. Wakuu wa Israel wanatumia vibaya matatizo ya kiuchumi ya Afrika na ukosefu wa ajira kujipenyeza katika bara hilo kwa madai ya kusuluhisha matatizo yake. Hivi sasa Waisraeli wanatekeleza miradi kadhaa ya kilimo, maji na uzalishaji umeme Afrika ili kujipendekeza kwa nchi za Kiafrika.

Aliza Bin-Noun balazo wa zamani wa Israel huko Ufaransa  anasema mabadilishano ya kibiashara baina ya Israel na Afrika ni ya takribani dola bilioni moja na milioni 200 na kusema: "Mashirika ya Israel yanashiriki katika miradi mbali mbali Afrika kama vile nishati jadidika, mawasiliano, kilimo na tiba."

Kustawi uhusiano wa kijeshi na kiusalama ni sekta nyingine inayofuatuliwa na watawala wa Israel barani Afrika. Wakuu wa Israel wanalenga kulitumia bara la Afrika kwa maslahi yao ya kijeshi. Hivi sasa bara la Afrika limegeuka na kuwasoko kubwa la silaha na zana za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha utawala huo ghasibu pia unatoa mafunzo ya kijeshi na kiusalama kwa nchi nyingi za Afrika mbali na kujenga vituo vya kijeshi katika visiwa vya Bahari ya Sham ambavyo ni milki ya Eritrea.

Netanyahu akikagua gwaride, Israel inalenga kujipenyeza kijeshi barani Afrika

Khalid Qadoumi, mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas mjini Tehran anasema, utawala wa Kizayuni unahusika na biashara haramu barani Afrika na maeneo mengine duniani.

Ingawa wakuu wa Israel wanalenga kuendeleza sera zao barani Afrika lakini inaelekea kuwa, kwa kuzingatia masaibu ambayo nchi za Afrika zilipata katika zama za ukoloni na kwa kuzingatia utambulisho bandia na wa kibaguzi wa Israel, utawala wa kikoloni wa Tel Aviv hautaweza kufanikisha melengo yake Afrika kama unavyokusudia.

 

Tags

Oct 16, 2017 12:52 UTC
Maoni