• Baada ya mashinikizo, Rais Mugabe apokonywa ubalozi mwema wa WHO

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amepokonywa wadhifa wa balozi mwema wa Shirika la Afya Duniani WHO ikiwa ni siku chache tu tangu kuteuliwa kwake, kufuatia mashinikizo ya kila upande yaliyopinga uteuzi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametangaza kufuta uamuzi wa awali uliomtangaza Rais Mugabe kuwa balozi mwema wa shirika hilo la kimataifa la afya.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mashinikizo ya wafadhili na mashirika ya haki za binadamu ndiyo yaliyolifanya Shirika la Afya Duniani litengue uamuzi wake wa awali.

Nchi za Magharibi zinamlaumu Mugabe kuwa ameharibu uchumi wa Zimbabwe na amefanya ukiukaji wa haki za binadamu katika utawala wake wa miaka 37. 

Shirika la Afya Duniani (WHO)

Akihutubia mkutano wa WHO uliofanyika huko Uruguay na kisha kumtangaza Mugabe kuwa balozi mwema wa magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika, Tedros Adhanom aliiisifu Zimbabwe kuwa ni nchi inayotoa kipaumbele kwa huduma za afya kwa wote ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma hizo.

Wanaokosoa Rais Mugabe kuteuliwa katika wadhifa huo wanasema kuwa, katika kipindi cha miaka 37 ya utawala wake nchini Zimbabwe, huduma za afya zimekuwa mbaya ambapo wahudumu wa afya wamekuwa hawalipwi mishahara mara kwa mara na kumekuwa na ukosefu mkubwa wa dawa muhimu.

Hata hivyo takwimu za WHO zinaonyesha kuwa, Zimbabwe ni nchi inayotoa kipaumbele kwa huduma za afya kwa wote ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma za afya.

Oct 22, 2017 14:36 UTC
Maoni