• UN na AU zatoa wito wa amani kabla ya uchaguzi wa marudio Kenya

Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimetoa taarifa ya pamoja zikitoa wito kwa wanasiasa na polisi nchini Kenya kuzingatia sheria katika kutatua mgogoro uliopo nchini humo.

Katika taarifa ya pamoja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat wamewataka viongozi wote kuunga mkono amani na wahakikishe uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria. Aidha wamewataka wanasiasa na wafuasi wao waandae mazingira ya amani na wajiuepushe na kuibua ghasia na machafuko.

Uchaguzi wa rais wa marudio nchini Kenya unafanyika Alhamisi wiki hii, baada ya Mahakama ya Kilele kubatilisha uchaguzi wa Agosti nane baada ya kinara wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga kuwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee. Hivi sasa chama cha Jubilee kinasisitiza uchaguzi uendelee kama ulivyopangwa lakini muungano wa NASA unasema uchaguzi wa marudio bado haujatimiza masharti ya kuufanya uwe huru na wa haki. Odinga ametoa wito kwa wafuasi wake kususia uchaguzi huo.

Raila Odinga (kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta

Wakati huo huo Rais Kenyatta amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Odinga lakini baada ya uchaguzi wa Alhamisi. Aidha amesema atatia saini muswada wa sheria mpya ya uchaguzi iliyofanyiwa marekebisho. Wapinzani wamepinga marekebisho hayo. Kenyatta amesema kuna usalama wa kutosha kwa ajili ya uchaguzi wa Alhamisi huku akitoa wito kwa wale ambao hawataki kupiga kura wasiwazuie wale wanaotaka kupiga kura.

 

Tags

Oct 23, 2017 13:54 UTC
Maoni