• Mugabe apewa kinga ya kutoshtakiwa, adhaminiwa usalama wake ndani ya Zimbabwe

Aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amepewa kinga ya kutoshtakiwa sambamba na kudhaminiwa usalama wake ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Duru za karibu na mazungumzo yaliyopelekea Mugabe kukubali kuachia madaraka zimefichua kuwa, kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93 aliomba kuendelea kuishi Zimbabwe na kupewa usalama.

Vyanzo hivyo vya habari vilivyonukuliwa na shirika habari la Reuters vimesema kuwa, Mugabe alisema: "Sitaki kwenda kuishi uhamishoni, ninataka kufia hapa Zimbabwe."

Mugabe na mkewe Grace

Habari zaidi zinasema kuwa, Mugabe pamoja na familia yake akiwemo mkewe Grace Mugabe watadhaminiwa usalama wao ndani ya Zimbabwe, na wapo huru kufanya safari nje ya nchi.

Juzi Jumanne, Mugabe alisalimu amri na kukubali kujiuzulu, kufutia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.

Hapo jana, Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu nyekundu hivi karibuni na Mugabe alirejea nchini akitokea Afrika Kusini, na anatazamiwa kuapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo kesho Ijumaa.

Emmerson Mnangagwa

 

Tags

Nov 23, 2017 14:27 UTC
Maoni