• Waziri wa Mambo ye Nje wa Zambia ajiuzulu kulalamikia ufisadi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kulalamikia kashfa za ufisadi zinazoizunguka serikali ya Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo.

Katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Harry Kalaba amesema amelazimika kuachia wadhifa huo alioushika kwa miaka minne, kutokana na zimwi la ufisadi linaloitafuna nchi hiyo, mbele ya kimya cha maafisa wakuu wa chama tawala Patriotic Front.

Kalaba ameandika: "Hatuwezi kuendelea kusimamia masuala ya taifa kwa mikwaruzano baridi, wakati ambapo kiwango cha ufisadi kiko juu, ufisadi unaofanywa na wale wanaopaswa kuupiga vita. Ni kana kwamba Wazambia maskini sio wao tena sababu ya sisi kuwako uongozini."

Kalaba aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2014 wakati wa utawala wa marehemu Rais Michael Sata na akaendelea kuushikilia chini ya Rais Lungu. 

 

 

Rais Edgar Lungu wa Zambia

Ni vyema kukumbusha kuwa, uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Agosti mwaka 2016 huko Zambia ulikuwa na ushindani mkali kati ya Lungu na kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema ambaye alidai kuibiwa kura.

Itafahamika kuwa, Zambia ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

 

Jan 03, 2018 15:17 UTC
Maoni