• Gaidi wa Boko Haram ajiripua na kuua watu 14 msikitini nchini Nigeria

Mtu aliyejifunga bomu mwilini amejiripua na kuua watu wasiopungua 14 ndani ya msikiti mmoja katika mji wa Gamboru ulioko kwenye jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria leo.

Ali Mustafa, mfanyakazi wa mashirika ya utoaji misaada amesema, gaidi huyo anayeaminika kuwa mwanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram alifanya shambulio hilo muda mfupi kabla ya Sala ya Alfajiri.

Mustafa amevieleza vyombo vya habari kuwa: "nilikuwa njiani nakwenda kusali Sala ya Alfajiri, mara nikasikia sauti ya mripuko mkubwa wa bomu ndani ya msikiti."

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, msikiti huo karibu wote ulibomolewa na kuteketea kwa moto. Ameongeza kuwa baada ya kupita saa kadhaa, walipoanza kuwatoa watu waliona maiti 14 ikiwemo ya mshambuliaji huyo.

Ripoti zinaeleza kuwa maiti zilikuwa zimetapakaa; na karibu jengo lote la msikiti liligeuka kifusi na kubakia vipande vichache tu vya kuta zilizosimama. Kwa mujibu wa ripoti hizo kuna uwezekano idadi ya watu waliouawa itaongezeka.

Moja ya hujuma za kigaidi zilizofanywa na Boko Haram

Japokuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram halijatoa tamko lolote hadi sasa la kutangaza kuhusika na jinai hiyo, lakini kundi hilo lililoanzisha uasi mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka Magharibi huwa kwa kawaida linawatumia watu wanaojiripua wakiwemo wanawake na wasichana kufanya mashambulio ya aina hiyo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama misikitini na masokoni.

Licha ya sisitizo la mara kwa mara linalotolewa na serikali ya Nigeria na jeshi lake kwamba limeshalishinda kundi la kigaidi la Boko Haram, kundi hilo la kitakfiri lingali linaendelea kufanya mashambulio ya mauaji yanayolenga wanajeshi pamoja na raia.

Wiki iliyopita raia wanne waliuliwa katika shambulio linaloaminika kufanywa na Boko Haram katika mji wa Maiduguri ambao ni kitovu cha juhuma na mashambulio ya kundi hilo la kigaidi.

Aidha mwezi Novemba uliopita mashambuliaji aliyejifunga mada za miripuko aliua watu wasiopungua 50 msikitini katika moja ya mashambulio makubwa zaidi kufanywa na Boko Haram katika miaka ya karibuni nchini Nigeria.../

Tags

Jan 03, 2018 15:33 UTC
Maoni