• Mahakama Tanzania yawatupa jela walionaswa na dhahabu na kutaifisha mali zao

Mahakama ya Dar es Salaam nchini Tanzania imewahukumu wafanyabiashara wawili kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya kiasi cha Shilingi milioni sita.

Watuhumiwa hao ambao ni Naushad Mohammed Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha vipande saba vya madini ya dhahabu  vyenye thamani ya Shilingi milioni 989.7 bila ya kuwa na leseni. 

Vipande vya dhahabu

Kadhalika mahakama hiyo imetaifisha dhahabu yote iliyokamatwa pamoja na mabegi mawili ya fedha kutoka nchi 15 duniani walizokamatwa nazo watuhumiwa hao. Watuhumiwa hao walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume visiwani Zanzibar tarehe 29 Novemba mwaka jana wakielekea Dubai. Hukumu hiyo ilitolewa Alhamisi ya jana, Januari 11 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yanayowakabili. Wafanyabiashara hao maarufu  ambao ni wakazi wa Zanzibar, walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili ambayo ni kula njama na  kusafirisha madini nje ya nchi kinyume cha sheria na bila kuwa na leseni kutoka mamlaka husika za serikali ya Dar es Salaam.

Uchimbaji dhahabu nchini Tanzania

Hadi sasa serikali ya Tanzania imenasa idadi kubwa ya dhahabu zikiwa zinasafirishwa nje ya nchi katika maeneo tofauti ya taifa hilo, huku watuhumiwa wake wakihukumiwa na mahakama. Usafirishaji kinyemela wa rasilimali hizo umekuwa ukiikosesha pato kubwa nchi hiyo na hivyo kuifanya iendelee kuwa masikini kwa muda mrefu licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini.

Tags

Jan 12, 2018 08:01 UTC
Maoni