Jan 13, 2018 14:21 UTC
  • Umoja wa Afrika wamtaka Rais wa Marekani awaombe radhi Waafrika

Umoja wa Afrika AU umemtaka Rais wa Marekani Donald Trump aombe radhi kutokana na matusi na kejeli zake dhidi ya Waafrika.

Umoja wa Afrika sambamba na kulaani vikali matusi na kejeli hizo za Trump umesema kuwa, Rais wa Marekani anapaswa kuwaomba radhi Waafrika baada ya kuwatusi na kuwakejeli.

Ebba Kalondo, msemaji wa Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema kuwa, matamshi hayo ya Trump katu hayakubaliki na yamewavunjia heshima Waafrika.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema kuwa, matamshi yalitolewa na Trump hayana heshima. Taarifa hiyo aidha imesisitiza kwamba: Sambamba na kuonyesha kushangazwa kwetu , Umoja wa Afrika unaamini  kwamba, serikali mpya ya  Marekani hailielewi bara la Afrika na watu wake.

Rais Donald Trump wa Marekani

Sehemu nyingine ya taarifa ya Umoja wa Afrika imesema: Matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu bara Afrika yanaonyesha ubaguzi wa wazi alionao Rais huyo.

Wakati huo huo, jana Ijumaa, mabalozi wa nchi 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa walitoa tamko la pamoja na kulaani matusi na matamshi ya kibaguzi na ya kudhalilisha ya Rais wa Marekani, Donald Trump aliyoyatoa dhidi ya nchi za Afrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika na kumtaka aombe radhi rasmi na afute matusi yake.

Juzi Alkhamisi, Trump alitoa matusi makali dhidi ya Waafrika na nchi za Amerika ya Latini za Haiti na El Salvador kwa kuziita nchi hizo kwamba ni "Shimo la Kinyesi".

Maoni