• Rwanda yasisitiza kuhusu azma ya kustawisha uhusiano na Iran

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema nchi yake imekusudia kustawisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja zote.

Kagame ameyasema hayo wakati akipokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Iran nchini Rwanda Morteza Mortazavi.

Mbali na kukaribisha uwekezaji wa mashirika ya Kiirani katika miradi ya maendeleo nchini Rwanda, Rais Kagame ametaka pia kuimarishwa uhusiano baina ya sekta za binafsi za nchi mbili.

Kwa upande wake, balozi mpya wa Iran anayewakilisha nchi kadhaa ikiwemo Rwanda, mbali na kukabidhi hati zake za utambulisho, amefikisha pia salamu na ujumbe wa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mwenzake wa Rwanda wa kuitembelea Iran, na kueleza kwamba viongozi wa Tehran wana azma ya dhati ya kustawisha uhusiano na nchi za Afrika ikiwemo Rwanda.

Balozi mpya wa Iran nchini Rwanda Morteza Mortazavi (kulia) akikabidhi hati za utambulisho kwa Rais Paul Kagame

Balozi mpya wa Iran nchini Rwanda ambaye anaiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda mbali na kumpongeza Rais Kagame kwa kuchaguliwa tena kuwa rais na kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU) wadhifa anaotazamiwa kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi huu na pia kwa Rwanda kuwa mwanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, ametilia mkazo pia ushirikiano wa Tehran na Kigali katika jumuiya za kikanda na kimataifa ukiwemo Umoja wa Afrika.

Katika mazungumzo hayo na Kagame, Morteza Mortazavi ameashiria uwezo wa mashirika ya Kiirani katika nyanja mbalimbali na kutangaza utayari wa sekta binafsi ya Iran kutekeleza miradi ya ustawi na maendeleo nchini Rwanda.../

 

Tags

Jan 19, 2018 07:48 UTC
Maoni