Feb 09, 2018 14:18 UTC
  • Ethiopia yaendelea kuwaachia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa

Mwanasheria Mkuu wa Ethiopia ametoa agizo la kuachiwa huru mamia ya wafungwa wa kisiasa, akiwemo mmoja wa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo.

Shirika la habari la serikali la FANA limetangaza kuwa, agizo hilo la kuachiwa huru wafungwa 746, akiwemo Andualem Arage, kinara wa upinzani nchini humo ambaye kukamatwa kwake kulilalalamikiwa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama Human Rights Watch na Amnesty International, lilitolewa jana Alkhamisi.

Zaidi ya wafungwa 400 walioachiwa huru walikuwa 'wamepatikana na hatia' ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi, kueneza misimamo mikali iliyochupa mipaka na kuchochea machafuko, miongoni mwa jinai nyingine.

Hivi karibuni, serikali ya Ethiopia iliendeleza wimbi la kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, ambapo iliwaondoa gerezani wafungwa 2,345 waliotuhumiwa kuhusika na machafuko yaliyolikumba eneo la Oromiya kati ya 2015 na 2016.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn

Hivi karibuni, Merara Gudina, kiongozi mwingine wa chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress ambaye alikamatwa mwaka jana aliporejea kutoka Ulaya, wakati nchi hiyo ilikuwa chini ya sheria ya hali ya hatari, aliachiwa huru pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wapatao 115.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn alitangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa, kwa lengo la 'kuhuisha' demokrasia halisi nchini humo.

Tags

Maoni