• Rais Zuma wa Afrika Kusini apewa masaa 48 ajiuzulu

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amepewa masaa 48 awe ameachia ngazi, baada ya kufanyika mkutano wa dharura wa chama tawala ANC.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa amemkabidhi Zuma ilani ya kujiuzulu, baada ya kumalizika kikao cha jana cha Baraza Kuu la ANC.

Uamuzi wa jana umefikiwa baada ya Zuma na Ramaphosa kufanya mazungumzo ya siku tano kuhusu hatima ya Rais huyo wa Afrika Kusini anayeandamwa na kashfa za ufisadi, bila kufikia natija yoyote.

Rais Jacob Zuma amezidi kuwa chini ya mashinikizo ya chama tawala cha ANC tangu Cyril Ramaphosa alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Rais Zuma na Ramaphosa

Awali ANC ilikuwa imegawika baina ya waungaji mkono wa Zuma na wapinzani wake, jambo ambalo liliwafanya washindwe kumlazimisha Jacob Zuma ajiuzulu kabla ya kumalizika kipindi chake cha urais mwakani.

Iwapo Jacob Zuma atajiuzulu, Cyril Ramaphosa ambaye ni makamu wake atachukua uongozi wa Afrika Kusini hadi utakapoitishwa uchaguzi mwingine wa rais kati kati ya mwaka ujao 2019.

Tags

Feb 13, 2018 03:10 UTC
Maoni