• Kupatiwa Rais Zuma wa Afrika Kusini masaa 48 ya kujiuzulu

Kufuatia kushtadi mgogoro nchini Afrika Kusini, chama tawala cha cha ANC kimempatia Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo masaa 48 ili ajiuzulu au ajiandae kuachia ngazi.

Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa amemkabidhi  Rais Zuma ilani ya kujiuzulu, baada ya kumalizika kikao cha jana cha masaa manane cha Baraza Kuu la ANC.

Uamuzi wa jana umefikiwa baada ya Zuma na Ramaphosa kufanya mazungumzo ya siku kadhaa kuhusu hatima ya Rais huyo wa Afrika Kusini anayeandamwa na kashfa za ufisadi, bila kufikia natija yoyote.

Utendaji wa Rais Zuma kwa muda sasa umekuwa ukikosolewa na kulalamikiwa mno na wapinzani pamoja na vyama mbalimbali vya kisiasa vya nchi hiyo. Tangu Zuma aingie madarakani mwaka 2009 hadi sasa, amekuwa akiandamwa na kashfa mbalimbali za ufuska na utakatishaji pesa. Licha ya kuwa Zuma amekanusha tuhuma hizo na wakati mwingine kuahidi kupambana na wahalifu katika uwanja huo, lakini hadi sasa ameshindwa kuwaridhisha wapinzani na hata washirika wake wa zamani.

Rais Jacob Zuma  akiwa na Cyril Ramaphosa, mwenyekiti wa ANC

Tuhuma hizo zimewafanya wapinzani kwa nyakati tofauti wafanye juhudi za kumuondoa madarakani Rais Zuma. Kuwasilishwa mpango wa kumsaili bungeni mwaka jana ni miongoni mwa juhudi za wapinzani za kumuondoa madarakani Rais Zuma zilizogonga ukuta. Pamoja na hayo, kushadidi mashinikizo dhidi ya Zuma, mara kadhaa kumemlazimisha alifanyie mabadiliko baraza lake la mawaziri kama njia ya kupunguza mashinikizo hayo. Hata hivyo hatua yake ya kumfuta kazi Pravin Gordhan, aliyekuwa waziri wa fedha ilikabiliwa na upinzani mkubwa. Aidha Zuma alitangaza habari ya kuunda kamati maalumu ya kimahakama kwa ajili ya kufuatilia ufisadi na kupambana nao pia.

Licha ya hatua zote hizo, kuzidi kuwa mbaya hali ya uchumi na kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira nchini Afrika Kusini ni mambo ambayo yameongeza mashinikizo dhidi ya Rais Zuma, kiasi kwamba, viongozi wengi wa chama chake cha ANC sasa wameingiwa na wasiwasi wa kupoteza nafasi zao. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Disemba mwaka jana, chama tawala cha ANC kilimuondoa Zuma katika wadhifa wa mwenyekiti wa chama na kumpatia nafasi hiyo  Cyril Ramaphosa.

Nembo ya chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC

Katika hotuba yake ya kwanza akiwa kama mwenyekiti wa ANC, Ramaphosa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini alisisitiza juu ya kutekeleza mageuzi ya kiuchumi nchini humo na kwamba, chama hicho kitapambana na wahalifu wa kiuchumi serikalini na katika sekta binafsi.

Hivi sasa mazingira yanayotawala nchini Afrika Kusini yako kwa namna ambayo, sio tu kwamba, wapinzani wa serikali ndio wanaotaka kujiuzulu Rais Zuma bali, kundi kubwa la washirika wa Zuma katika kipindi cha mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid, viongozi wa jumuiya za wafanyakazi na asasi za kiraia nchini humo nao wamekuwa wakimshinikiza Zuma ajiuzulu.

Kwa mujibu wa uamuzi wa chama tawala cha ANC sasa Zuma ana muda mchache wa masaa 48 tuu ajiuzulu na kuachia hatamu za uongozi. Baadhi ya duru zinafichua kwamba, tayari Rais Zuma amekubali kujiuzulu lakini ametoa masharti na sharti kuu ni kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa. Hata hivyo Cyril Ramaphosa amekanusha taarifa za kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa Rais Zuma endapo atajiuzulu.

Weledi wa mambo wanaamini, vyovyote itakavyokuwa, endapo Zuma atajiuzulu, mrithi wake atakuwa na kibarua kigumu cha kurekebisha mambo hususan uchumi uliozorota wa nchi hiyo.

Tags

Feb 13, 2018 13:08 UTC
Maoni