Feb 14, 2018 12:36 UTC
  • Kuendelea radiamali ya mashirika ya haki za binadamu kuhusiana na udikteta wa uchaguzi nchini Misri

Katika radiamali ya hivi karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa kuhusiana na mchakato wa uchaguzi wa Rais nchini Misri, asasi na juumuiya kadhaa za haki za binadamu likiwemo Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch na waandishi wa habari wasio na mipaka zimetangaza kuwa, uchaguzi huo hauna hata vigezo vya chini kabisa vya kufanyika zoezi la upigaji kura katika mazingira ya wazi na huru.

Gazeti al al-Quds al-Arabi limetangaza katika ripoti yake kwamba, serikali ya Misri inayoongozwa na Rais Abdul-Fattah al-Sisi imezoea kutokomeza uhuru wa kisiasa katika nchi hiyo na ni kwa msingi huo ndio maana imekuwa ikiwatia mbaroni wagombea waliotangaza nia ya kuwania kiti cha urais pamoja na wafuasi wao. 

Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo imekosoa vikali hatua ya vyombo vya dola ya kukanyaga uhuru na haki za wananchi, sambamba na kuwatia mbaroni au kuwatishia wanasiasa walioonyesha nia ya kugombea urais.

Katika siku za hivi karibuni maafisa wa serikali ya Misri wamekuwa wakikandamiza viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na uhuru wa kijamii. Kwa miezi kadhaa sasa Misri imekuwa ikitawaliwa na anga ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa tatu tangu kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Bango la picha ya Rais al-Sisi anayegombea tena kiti cha urais wa Misri

Habari inayogonga vichwa vya habari zaidi kuhusiana na matukio ya Misri kwa sasa ni ya kufutwa wapinzani wa Jenerali al-Sisi wanaojitokeza na kutangaza nia ya kushindana na rais huyo katika uchaguzi ujao. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hatua hiyo inalenga kumuandalia mazingira Rais Abdul-Fattah al-Sisi ya kuendelea kutawala. Mwenendo wa kuwaondoa wapinzani hao katika ulingo wa uchaguzi ulianza kwa Ahmad Shafiq Waziri Mkuu wa Misri wa kabla ya matukio ya 2011 ambaye kutokana na kuandamwa na mashinikizo alisalimu amri na kuamua kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.

Muhanga mwingine alikuwa Khalid Ali, mwanasheria wa masuala ya haki za binadamu ambaye kutokana na kuandamwa na tuhuma za kimahakama alilazimika kujitoa katika kugombea kiti cha urais. Khalid Ali alijitoa kwenye uchaguzi huo siku moja tu baada ya kutiwa mbaroni Sami Hafez Anan mkuu wa zamani wa majeshi ya Misri. Inaelezwa kuwa, kosa lake lilikuwa ni kutangaza nia ya kugombea urais bila ya idhini ya serikali. Baada ya kutiwa mbaroni jenerali huyo wa jeshi, jina lake liliondolewa katika orodha ya wagombea urais.

Hatua hiyo ilifuatiwa na radiamali na malalamiko makubwa ya kimataifa kuhusiana na anga ya uchaguzi ya Misri ambayo inaonekana kuwakandamiza na kuwaondoa katika ulingo wa uchaguzi wagombea wote wanaoonekana kuwa wanaweza kuwa tishio kwa Rais al-Sisi. Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limetangaza kuwa, kutiwa mbaroni Sami Anan ni ukiukaji wa wazi wa haki ya mtu kushiriki katika uchaguzi na kuwataka watawala wa Misri kutoegemea upande wowote na kujiepusha pia na suala la kutaka kuweko mgombea mmoja tu wa kiti cha urais katika uchaguzi ujao.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye ameonyesha radiamali yake na kusema kwamba, ana matumaini Misri itashuhudia uchaguzi huru na wa haki. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua za kuwaondoa katika ulingo wa uchaguzi wagombea wengine, kivitendo zinaifanya Misri iwe katika mazingira ya mgombea mmoja.

Licha ya kuwa, Katiba ya Misri inaidhinisha kuweko hata mgombea mmoja wa kiti cha urais, lakini serikali ya Abdul-Fattah ikiwa na lengo la kujikosha na kupunguza mashinikizo ya ndani na ya kimataifa imepitisha jina la Moussa Moustafa Moussa kiongozi wa chama cha Ghad kuchuana na Rais al-Sisi katika uchaguzi ujao wa Rais mwezi ujao.

Hatua hiyo inaelezwa na weledi wa mambo kuwa ni mchezo wa kuigiza wa demokrasia. Katika upande mwingine shakhsia wengi wa Misri akiwemo Abdel Moneim Aboul Fotouh aliyegombea uchaguzi uliopita, Hashim Janan na Muhammad Anwar Sadat wameususia uchaguzi huo wakilalamikia kutokuweko uwezekano wa kufanyika kwake katika mazingira salama, ya wazi na huru.

Tags

Maoni