• Watu watano wafariki dunia katika ajali ya msafara wa rais wa Kongo DR

Kwa akali watu watano wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha msafara wa rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Habari zinasema kuwa ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Matadi kwenye eneo la Kimpese kusini magharibi mwa nchi hiyo. Eneo hilo liko umbali wa kilometa 220, kusini mwa mji mkuu Kinshasa. Ofisi ya Rais Kabila imetangaza leo kwamba, ajali hiyo imetokea wakati rais huyo alipokuwa anarejea mjini Kinshasa na kwamba mbali na watu watano kupoteza maisha, wengine 11 wamejeruhiwa.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Kadhalika taarifa hiyo ya ofisi ya rais imesema kuwa, miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo waliopoteza maisha ni askari watatu wa gadi ya rais na raia wawili. Msemaji wa ofisi ya Rais Kabila ameongeza kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni utelezi uliosababishwa na mvua kali zinazoendelea kunyesha.

Barabara za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinatajwa kuwa na miundombinu dhaifu mno ambapo baada ya kunyeshewa na mvua huwa hujaa utelezi ambao aghlabu husababisha ajali. Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili kama madini ya dhahabu na alimasi, lakini bado nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika imeendelea kugubikwa na umasikini wa kupindukia.

Tags

Feb 14, 2018 16:44 UTC
Maoni