Feb 14, 2018 16:50 UTC
  • Wakimbizi 33 wengine wapoteza maisha nchini Libya

Duru za kuaminika nchini Libya zimetangaza habari ya kuuawa wakimbizi zaidi ya 30 katika ajali ya barabarani nchini humo.

Duru hizo za kuaminika za Libya zimetangaza kuwa, watu 33 wamepoteza maisha katika ajali ya barabarani baada ya lori lililokuwa limewabeba wakimbizi hao kupata ajali na kupinduka.

Hata hivyo duru hizo hazikutoa taarifa zaidi kuhusu sababu za ajali hiyo wala uraia na wasifu wa wakimbizi waliokuwemo kwenye lori hilo.

Waafrika wanaohatarisha maisha yao kuelekea Ulaya kupitia Libya wanakumbana na mashaka na hatari nyingi

 

Libya hivi sasa imekuwa njia kuu ya magendo ya binadamu na ndiyo njia kuu inayotumiwa na Waafrika wanaokimbilia barani Ulaya kupata hifadhi.

Magendo ya binadamu yana faida kubwa za kifedha kwa magenge yanayofanya magendo hayo.

Kila mwaka makumi ya maelfu ya wahajiri wanapelekwa kimagendo barani Ulaya kupitia Libya baada ya kutoa fedha nyingi kwa magenge hayo.

Hata hivyo sehemu kubwa ya wakimbizi hao hawafiki waendako kwani huishia mikononi mwa magenge mengine ya binadamu na kupigwa mnada kama bidhaa sokoni, au wanapoteza maisha baharini kutokana na kutumia boti dhaifu mno kuelekea Ulaya au wanakufa kwa makumi katika ajali kama hizo za barabarani.  

Tags

Maoni