Feb 14, 2018 16:51 UTC
  • ANC yamuonya kwa mara mwisho Jacob Zuma

Chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini kimetoa onyo kali kwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo kwamba kitatumia nguvu za Bunge kumng'oa madarakani.

Onyo hilo limekuja muda mchache baada ya Rais Zuma kuzungumza na Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC) na kutangaza wazi kuwa hana nia ya kujiuzulu akisisitiza kuwa hakuna ovu lolote alilofanya la kumlazimisha aachie madaraka kabla ya kumalizika muda wa urais wake. Muda wa urais wa Jacob Zuma unamalizika mwaka ujao wa 2019.

Viongozi wa ANC wamesema leo Jumatano mara baada ya matamshi hayo ya Zuma kuwa wanaweza kupeleka muswada bungeni wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na hivyo kumuondoa kwa nguvu madarakani, tishio ambalo limezidi kumuweka kwenye mashinikizo rais huyo ambaye wakati fulani alikuwa mtu mwenye nguvu zaidi huko Afrika Kusini.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anayekabiliwa na mashinikizo makubwa ya kujiuzulu kabla ya kumalizika muda wake wa urais

 

Zuma amenukuliwa na shirika la habari la SABC akisema: "Hakuna chochote kibaya nilichofanya. Sidhani kwamba ninatendewa haki. Nimekuwa muhanga." 

Kabla ya hapo chama cha ANC kilikuwa kimempa Rais Zuma muhula wa masaa 48 wa kutangaza kujiuluzu. Muhula huo ulitolewa baada ya chama tawala cha ANC kuitisha kikao cha dharura cha kujadili mustakbali wa Jacob Zuma.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afrika Kusini, muhula huo ulitolewa baada ya  Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye ndiye mwenyekiti taifa wa ANC hivi sasa kumkabidhi Zuma ilani ya kujiuzulu, baada ya kumalizika kikao cha dharura cha Baraza Kuu la ANC jana Jumanne.

Maoni