• Maisha nchini Kenya yatabiriwa kuendelea kuwa magumu kutokana na kuendelea hali ya ukame

Gharama ya maisha kwa raia wa Kenya inatazamiwa kupanda zaidi kutokana na kurefuka kipindi cha kiangazi na ongezeko la bei za mahitaji muhimu ya kuzalisha bidhaa.

Taarifa zinasema, kwa miezi kadhaa sasa, gharama za uzalishaji wa umeme zimekuwa zikiongezeka mara dufu nchini humo kufuatia kukosekana kwa maji ya kutosha katika vituo vya kuzalisha nishati hiyo muhimu. Mbali na hayo, bei ya mafuta ambayo ni hitaji lingine muhimu kwa ajili ya kuzalisha bidhaa muhimu pia inazidi kupanda.

Hali ya ukame nchini Kenya

Hivi karibuni Waziri wa Nishati, Charles Keter, alinukuliwa akisema kuwa, upungufu wa maji katika vituo vya kuzalishia umeme unazidi kuongezeka kwa kiwango cha kutia wasiwasi. Suala hilo limeibua hofu kwa wananchi juu ya uwezekano wa kutozwa gharama zaidi za umeme endapo mvua haitanyesha hivi karibuni. Waziri wa Nishati, Charles Keter aliyeyasema hayo baada ya kuzuru kituo cha kuzalisha umeme cha Sondu-Miriu katika Kaunti ya Kisumu, siku ya Jumatano iliyopita aliongeza kuwa, serikali imelazimika kutumia mbinu ghali zaidi za kuzalisha umeme kwa kiwango kinachohitajika. Kabla ya hapo pia Keter alisema kuwa huenda serikali ikalazimika kufunga kituo kingine cha Masinga kutokana na upungufu wa maji katika bwawa la Masinga nchini humo.

Waziri wa Nishati nchini Kenya, Charles Keter.

Kituo hicho huzalisha Megawati 40 za umeme. Hata hivyo, aliwapa matumaini Wakenya kwamba msimu wa mvua wa mwezi Machi hadi Mei unatarajiwa kuleta ahueni wiki mbili zijazo. Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumatano iliyopita, Tume ya Kudhibiti Nishati nchini Kenya (ERC), ilitangaza ongezeko mpya la bei za mafuta kwa mwezi wa sita mfululizo sasa, suala ambalo liliamsha hisia za raia wa taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kawaida bei ya mafuta ndio hutumika kutathmini hali ya uchumi kitaifa kwani kutokana na taathira yake katika gharama za maisha kwa wananchi.

Tags

Feb 16, 2018 04:51 UTC
Maoni