• Makumi wauawa katika mapigano ya kikabila mkoani Ituri Kongo

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza habari ya kuuliwa makumi ya watu katika mapigano ya kikabila katika mkoa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Huku likitegemea vithibitisho, shirika la Unicef jana Ijumaa lilitangaza kuwa watu 76 wengi wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyojiri katika mkoa wa Ituri kuanzia mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa. Taarifa ya Unicef imeongeza kuwa hatima ya watoto zaidi ya elfu 46 waliolazimika kuwa wakimbizi kufuatia mapigano hayo ya kikabila huko Ituri inatia wasiwasi. 

Hali halisi ya mapigano ya kikabila mkoani Ituri 

Mfuko huo wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa raia zaidi ya laki mbili wamekuwa wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni natija ya mapigano ya kikabila yaliyoanza tangu mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa mkoani Ituri. Ripoti ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa vijiji zaidi ya 70 pia vimechomwa moto katika machafuko ya karibuni huko Kongo. 

Ni miaka ishirini imepita sasa ambapo maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani.

Tags

Feb 17, 2018 02:43 UTC
Maoni