• Uchaguzi mdogo Tanzania wagubikwa na machafuko; CCM yaelekea kushinda

Polisi nchini Tanzania imethibitisha kuwa mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika vurugu zilizohusiana na uchaguzi mdogo wa bunge uliofanyika leo katika jimbo la Kinondoni lililoko katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha kuwa mtu mmoja alipigwa risasi jana wakati askari wa jeshi hilo walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa chama cha upinzani cha Chadema waliokuwa wanaandamana kuelekea ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Mtu huyo aliyeuawa ambaye ni mwanachuo ametambulika kwa jina la  Aquillina Akwilini.

Aquillina Akwilini

Hayo yamejiri katika hali ambayo, wakati zoezi la kuhesabu kura za jimbo lililokuwa na mchuano mkali la Kinondoni likiwa linaendelea matokeo ya awali yanaonyesha kuwa mgombea wa CCM Said Mtulia anaongoza kwa wingi wa kura dhidi ya mpinzani wake Salum Mwalimu wa Chadema.

Mbali na Kinondoni, uchaguzi mwengine mdogo wa bunge umefanyika katika jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro ambapo mgombea wa Chadema Elvis Christopher amechuana na Dkt. Godwin Ole Mollel wa CCM.

Chaguzi hizo zimeitishwa baada ya kujiuzulu wabunge wa zamani wa majimbo hayo.

Chaguzi nyingine ni za madiwani wa kata nane Tanzania Bara. Zaidi ya wapiga kura laki 3 na 55,000 waliandikishwa kupiga kura katika chaguzi hizo.../

Tags

Feb 17, 2018 17:17 UTC
Maoni