• Sisitizo la Fayez al-Sarraj kuhusu nafasi ya kura ya maoni katika kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini Libya

Waziri Mkuu wa serikali ya maridhiano ya kitaifa ya Libya amesisitiza kuwa: kufanyika kura ya maoni ya rasimu ya katiba kutakuwa na taathira kubwa katika kuhitimisha mkwamo wa kisiasa ulioitanza nchi hiyo.

Fayez al-Sarraj, ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa saba wa ushindi wa mapambano ya wananchi wa Libya yaliyouangusha utawala wa kidikteta wa Muammar Gaddafi. Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo wa serikali ya umoja wa maridhiano ya kitaifa ya Libya, kufikiwa maridhiano jumuishi na wenye wigo mpana ya kitaifa na kufanyika kura ya maoni ya rasimu ya katiba ndio njia pekee ya kuweza kuhitimisha mpasuko na mgawanyiko wa madaraka pamoja na mivutano na mkwamo wa kisiasa unaoendelea kuitanza nchi hiyo.

Muammar Gaddafi

Hotuba ya Al-Sarraj na sisitizo lake la kuitishwa kura ya maoni vimetolewa katika hali ambayo licha ya jitihada mbali mbali zilizofanywa na pamoja na kufanyika duru kadhaa za mazungumzo, Libya ingali inasokotwa na mgogoro wa kisiasa. Kuwepo chungu ya silaha mikononi mwa makundi tofauti ya wanamgambo, mvutiano wa mgao wa madaraka baina ya makabila na mirengo mbalimbali, uingiliaji wa siri na wa dhahiri wa maajinabi, kukosekana muundo imara wa kisiasa na kuwepo mfumo maalumu wa kikabila na kikoo ni miongoni mwa sababu za kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Libya. Hii ni katika hali ambayo kwa kuendelea hali hiyo, hivi sasa hatari ya kurejea magaidi nchini Libya na kujipenyeza kwenye maeneo na nchi nyengine jirani limekuwa tatizo sugu si kwa Libya pekee bali kwa eneo na dunia nzima. Ahmad Qadhaf Ad-Dam, afisa wa zamani wa serikali ya Libya anaizungumzia hali hiyo kwa kusema: Kila siku mamia ya wanachama wa Daesh, ambao wametoroka kutoka nchi za Syria na Iraq wanaingia nchini Libya kwa lengo la kuvuruga uthabiti ndani ya nchi.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh ambao wameshaingia na kupiga kambi nchini Libya 

Kwa kuzingatia hali hiyo, hivi sasa viongozi wa Libya wanafanya kila njia ili kuweza kupata ufumbuzi wa kivitendo wa kuinasua nchi hiyo na mgogoro wa kisiasa unaoikabili kwa njia ya kuitisha uchaguzi wa rais na bunge na vilevile kura ya maoni ya rasimu ya katiba.

Hata hivyo wachambuzi wanasema, kutokana na mazingira yaliyopo, kuna vikwazo na vizuizi kadhaa vinavyotatiza mchakato wa zoezi la uchaguzi nchini Libya.  Ghassan Salamé, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya anaizungumzia hali hiyo kwa kusisitiza kuwa, mazingira hayajakamilika kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi nchini Libya. Salamé amesema: Kwa sasa tumeweza kukamilisha awamu moja tu kwa ajili ya kuitisha uchaguzi, ambayo ni uandikishaji wapiga kura.

Ghassan Salamé (kushoto) akiwa na Fayez al-Sarraj

Kudhamini usalama wa ndani, kuyavunja makundi ya wanamgambo, kukusanya silaha na vilevile kuwahamasisha wananchi washiriki katika uchaguzi pamoja na pande zote husika kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo ni miongoni mwa changamoto muhimu zaidi zinazolikabili zoezi hilo. Kwa upande mwengine, akthari ya makundi na mirengo ya kisiasa nchini Libya inaitakidi kuwa kufanyika uchaguzi ndio njia itakayohitimisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa jeshi la taifa amesema kuhusiana na suala hilo kuwa: Inapasa uchaguzi uitishwe  haraka iwezekanavyo, japokuwa Libya bado haijawa na ukomavu wa kidemokrasia unaohitajika.

Alaa kulli hal, japokuwa hitilafu za mitazamo na mvutiano wa mgao wa madaraka baina ya mirengo ya kisiasa na kikabila vingali ni vizuizi vikubwa vya kupatikana mazingira ya kuitishwa uchaguzi, na licha ya matatizo yote yaliyopo, hivi sasa juhudi zote zinalenga kuharakishwa mchakato wa kuitishwa uchaguzi mkuu nchini Libya. Sababu ni kwamba wadau wote katika uga wa kisiasa nchini Libya wamefikia natija kwamba kuitisha uchaguzi na kurejea uthabiti wa kisiasa na usalama ndio njia itakayohitimisha mgogoro na kuweza kudhibiti hali ya mambo katika nchi hiyo.../ 

 

Tags

Feb 19, 2018 07:10 UTC
Maoni