• Sudan yawaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa

Serikali ya Sudan imewaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa kufuatia msamaha uliotolewa na Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.

Miongoni mwa wafungwa hao walioachiliwa huru wamo viongozi wa ngazi za juu wa chama cha Umma na wanasiasa wengine ambao walitiwa mbaroni hivi karibuni katika maandamano ya kulalamikia kupanda kwa bei za bidhaa nchini humo.

Taarifa zaidi kutoka Khartoum zinasema kuwa, serikali ya nchi hiyo imewaachilia huru takribani wanaharakati 80 wa upinzani waliokamatwa mwezi Januari wakati maafisa wa usalama walipokuwa wanajaribu kukandamiza maandamano na malalamiko dhidi ya kupanda kwa bei za vyakula.

Rais Omar Hassan al-Bashir

Mmoja wa viongozi wa karibu na Rais wa Sudan amesema kuwa, Rais al-Bashir ametoa agizo la kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa.

Idadi kubwa ya raia walionekana wakiwa wamekusanyika mbele ya mlango wa gereza la Kobar kwa ajili ya kuwapokea ndugu zao walioachiliwa huru.

Maandamano ya hapa na pale yamekuwa yakifanyika tangu Januari mwaka huu mjini Khartoum na miji mingine ya Sudan baada ya vyama vya upinzani na wanaharakati kutoa wito wa kufanyika maandamano dhidi ya serikali na kulalamikia kupanda kwa bei za vyakula.

  

Tags

Feb 19, 2018 07:54 UTC
Maoni