• Jeshi la Nigeria lashindwa kumkamata kinara Boko Haram

Vikosi vya jeshi la Nigeria vimeshindwa kumkamata kiongozi wa kundi la magaidi wakufurishaji la Boko Haram, Abubakar Shekau katika oparesheni maalumu iliyofanyika hivi karibuni.

Gazeti la Nigeria la Sahara Reporters limearifu kuwa, baada ya siku nne kuelekea ngome ya Shekau kaskazini mashariki mwa Nigeria, wanajeshi hao waliamriwa kusitisha safari yao ya kusonga mbele.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi, vikosi vya Nigeria vinajipanga upya tayari kushambulia ngome kuu ya Shekau kwa ili kumkamata kinara huyo wa magaidi akiwa hai.

Hata hivyo katika operesheni ya hivi karibuni, Shekau aliweza kutoroka wakati jeshi lilipokaribia eneo ambapo alikuwa, kwa mujibu wa chanzo hicho.

Serikali ya Nigeria wiki iliyopita imetangaza zawadi ya dola elfu nane kwa mtu atakayetoa taarifa za kuwezesha kukamatwa Abubakar Shekau, kiongozi Boko Haram.

Magaidi wakufurishaji

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu 20 elfu wameuawa. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo ambalo lina ufahamu usio sahihi na potofu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags

Feb 20, 2018 15:36 UTC
Maoni