• Rais Kabila amteua waziri mpya wa masuala ya ndani, usalama wazorota DRC

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteua mkuu wa chama chake cha kisiasa kuwa waziri mpya wa mambo ya ndani, kutokana na kushtadi ukosefu wa usalama na harakati za magenge ya waasi nchini humo.

Rais Kabila amemteua Henri Mova Sakanyi, Katibu Mkuu wa chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy PPRD, kurithi mikoba ya Emmanuel Ramazani Shadari, ambaye pia ni afisa wa ngazi za juu wa chama hicho tawala.

Makumi ya watu wameuawa na maafisa usalama katika maandamano ya kumshinikiza Kabila aachie ngazi, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Muhula wa pili na wa mwisho kikatiba wa Kabila ulimalizika Disemba mwaka 2016.

Haya yanajiri siku chache baada ya wafanyakazi wawili wa shirika moja la Ufaransa la kutoa misaada kuuawa katika mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku wa tatu akichukuliwa mateka katika kijiji cha Mushikiri katika mkoa wa Kivu Kaskazini. 

Maandamano dhidi ya Rais Kabila

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa amani na usalama katika mkoa wa Kivu Kaskazini na kusema hali hiyo inavuruga shughuli za utoaji misaada kwa maelefu ya wahitaji katika eneo hilo.

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, makundi mbalimbali ya waasi na wanamgambo yamekuwa yakiendesha shughuli zao katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tags

Feb 21, 2018 07:35 UTC
Maoni