• Asasi za kiraia Tanzania zataka kuundwa tume ya kuchunguza mauaji

Makundi ya kiraia nchini Tanzania yametoa wito wa kuundwa tume huru ya kuchunguza vifo ambavyo vimekuwa vikitokea nchini humo katika mazingira ya kutatanisha hasa katika siku za hivi karibuni.

Viongozi wa Asasi za Kiraia (Azaki) wamesema kuwa, tume hiyo inafaa kuwashirikisha maafisa wa AZAKI, Taasisi za Dini, Vyombo vya Habari, Baraza la Vyama vya Siasa, Wanahabari, Majaji/Mahakimu, Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Viongozi wa asasi hizo za kiraia wanasema kuwa, uchunguzi huru unahitajika kuhusu vifo na vitendo vya utekwaji na utesaji vilivyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, wameomba askari wanaotuhumiwa kuhusika kusababisha kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline wafikishwe katika vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe kwa aliyehusika na tukio hilo.

Mwanafunzi Akwilina Akwiline wa chuo cha NIT, aliyeuawa kwa risasi na polisi jijiji Dar es Salaam waliokuwa wakidhibiti maandamano ya chama cha Chadema

Taarifa ya viongozi hao wa asasi za kiraia Tanzania imesema kuwa, "Taifa liwe na mfumo huru au chombo huru cha kuchunguza na kusimamia mashtaka yanayohusu vyombo vya usalama badala ya kuwaachia wao kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka. 

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema, matukio yanayowahusu polisi kama watuhumiwa ni kosa kubwa kuwaachia wao wenyewe wajichunguze na hili limekuwa sasa chanzo cha matukio kuendelea kutokea na kutochukuliwa hatua katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Maafisa hao wa kutetea haki za kibinadamu wamesema kwamba, hali nchini Tanzania kwa sasa inasikitisha hasa kutokana na kuripotiwa mara kwa mara kutokea vifo vya kutatanisha. 

Viongozi hao wa Azaki wametoa wito kwa Serikali kutazama upya suala la upatikanaji wa Katiba mpya wakisema "ndiyo suluhisho la matatizo mbalimbali yanayotokea katika jamii nchi hiyo kwa sasa." Aidha, wameomba kuundwe Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Tags

Feb 21, 2018 15:21 UTC
Maoni