• Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
    Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Serikali ya Burundi imetoa taarifa mpya ya kukosoa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya kibinaadamu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana Alkhamisi na serikali ya Bujumbura, sambamba na kulaani vikali ripoti hiyo, imeutuhumu pia Umoja wa Mataifa kutokana na hatua yake ya kuandaa ripoti inayopendelea upande mmoja. Katika ripoti hiyo Burundi imesema kuwa, UN imependelea na haizingatii uhalisia wa mambo. Hii ni kusema kuwa, viongozi wa Burundi wanaamini kwamba, hali ya mambo nchini humo ni nzuri na kwamba kila hatua ya kimataifa inayotekelezwa kinyume na hali hiyo inafaa kupingwa.

Raia wa Burundi wakiandamana kulaani ripoti ya Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, watu milioni tatu na laki sita nchini humo, yaani kila mtu mmoja kati ya watatu, anahitajia misaada ya kibaadamu mwaka huu 2018. Ripoti hiyo ni ongezeko la asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na ile ya mwaka jana 2017.

Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Bujumbura kupinga na kukosoa ripoti za Umoja wa Mataifa ambapo katika uwanja huo viongozi wa Burundi wanaituhumu UN kuwa inatoa taarifa za upendeleo kuhusiana na hali ya mambo nchini humo. Hivi karibuni pia maelfu ya raia wa Burundi waliandamana mjini Bujumbura kulaani ripoti ya Michel Kafando, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi kuhusiana na hali ya mambo nchini humo.

Tags

Feb 23, 2018 14:35 UTC
Maoni