• Generali Kayihura aliyepigwa kalamu nyekundu na Rais Museven ashtakiwa ICC

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) aliyefutwa kazi hivi karibuni na Rais Yoweri Museven wa Uganda Kale Kayihura, ameshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na makosa dhidi ya binadamu ambayo inadaiwa aliyafanya alipokuwa na wadhifa huo wa polisi.

Taarifa inasema kuwa, Kayihura na washirika wake 16 walilirejesha kwa nguvu kundi la raia wa Rwanda kutoka Uganda, suala ambalo limetajwa kuwa lilikiuka haki za binaadamu dhidi ya watu huo. Kundi hilo likiongozwa na Rugema Kayumba limesema kwamba, limeamua kufungua kesi ya malalamiko mbele ya Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi kwa maelezo kwamba lilishindwa kupata haki muda mrefu nchini Uganda.

Rugema Kayumba, kushoto na Kale Kayihura

Aidha limeongeza kwamba makosa ya uhalifu aliyoyatenda Kayihura na washirika wake yamewasilishwa tayari mbele ya mahakama hiyo na kwamba imefungua aina nne ya mashtaka ambayo ni pamoja na uhalifu wa uvamizi, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari. Jenerali Kayihura alikuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda kwa zaidi ya miaka 12 ambapo alifutwa kazi siku ya Jumapili iliyopita na Rais Yoweri Museveni.  Katika mabadiliko hayo nafasi yake imechukuliwa na Okoth Ochola.

Rais Museven wa Uganda

Kayihura ameshtakiwa katika mahakama hiyo ya ICC pamoja na maofisa wengine 16 wa polisi  wakiwamo Mrakibu  Mandamizi wa Polisi (SSP)  Nixon Agasiirwe na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Aguma Joel. Malalamiko ya uhalifu yamefunguliwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu katika mahakama hiyo ya The Hague, Uholanzi. Mbali na hayo Kale Kayihura anakosolewa na wapinzani nchini Uganda kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwakandamiza wafuasi wa vyama vya upinzani hususan katika chaguzi zilizopita ambapo katika uwanja huo pia waliwahi kuwasilisha mashitaka dhidi yake.

Tags

Mar 07, 2018 14:27 UTC
Maoni