• Malengo ya Marekani barani Afrika

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amewasili Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia ikiwa ni kituo chake cha kwanza cha safari yake ya kiduru ya kuzitembelea nchi kadhaa za Kiafrika.

Mbali na Ethiopia, Rex Tillerson anatarajiwa kuzitembelea pia nchi za Kenya, Djibouti, Chad na Nigeria. Kabla ya kuanza safari yake hiyo barani Afrika, Tillerson alisema: Hakuna wakati usalama na kuchanua uchumi wa nchi yetu ulikuwa na mafungamano na Afrika kama ilivyo hii leo.

Pamoja na hayo, mbinu anayoitumia Rais Donald Trump katika kuamiliana na bara la Arika inaonyesha kuwa, serikali ya sasa ya Marekani haiheshimu hata viwango vidogo kabisa vya kidiplomasia. Hatua ya Rais wa Marekani ya mwanzoni mwa mwaka huu ya kuzihutubu nchi za Kiafrika na kuziita kuwa "Shimo la Choo" ililipua ghadhabu katika kila kona ya bara la Afrika. Katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa, nchi zote za Kiafrika zilitoa taarifa ya pamoja ya kulaani maneno hayo ya kibaguzi na lugha isiyo na heshima ya Trump na baadhi ya nchi za Kiafrika ziliwaita mabalozi wa Marekani katika nchi hizo na kuwakabidhi malalamiko yao.

Rex Tillerson, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani akiwasili Addis Ababa Ethiopia

Kabla ya hapo pia, marufuku ya Rais Trump kwa raia wa baadhi ya nchi za Kiafrika kama Somalia, Libya na Chad ya kufanya safari nchini Marekani nayo ilikuwa imekabiliwa na malalamiko makubwa ya nchi za bara hilo. Sambamba na hayo, Trump alitishia kuzikatia misaada nchi ambazo zingepinga hatua yake ya kuitambua Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Msimamo huo wa Trump ulifichua siasa za maji taka za Washington za kutumia vibaya matatizo ya kifedha ya nchi za Kiafrika. Reuben Brigety mjumbe na mwakilishi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Afrika anasema: Trump hajui mambo mengi kuhusiana na Afrika na inaonekana kwamba, alikuwa na hamu ya kufahamu kitu kuhusu nchi za bara hilo.

Tab'an, ili kushusha ghadhabu za nchi za Kiafrika zilizotokana na matamshi ya kibaguzi na kifidhuli ya Trump dhidi ya bara la Afrika, Tillerson alitangaza mwezi Januari kwamba, kwa mara ya kwanza ataelekea barani Afrika akiwa kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani. Hivi sasa Rex Tillerson ana matumaini kwamba, kwa kushusha ghadhabu na hasira za nchi za Kiafrika ataweza kuongeza kasi ya ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi wa nchi yake na bara la Afrika. Kupanuka wigo wa harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika, kuhamia mabaki ya kundi la kigaidi la Daesh katika maeneo mbalimbali ya Afrika na kushadidi ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na kijamii katika nchi za bara hilo na hivyo kuufanya mgogoro wa kibinadamu na wakimbizi kuwa mkubwa, ni baadhi ya mambo ambayo yanahesabiwa kuwa yameitia wasiwasi Marekani katika uga wa usalama.

Mradi wa China wa ujenzi wa reli ya umeme Addis Ababa Ethiopia

Marekani ina matumaini kwamba, katika mazingira haya ya kuzidi kuzorota hali ya ukosefu wa usalama barani Afrika itaweza kupanua zaidi kambi na vituo vyake vya kijeshi katika bara hilo na hivyo kukwamisha juhudi za washindani wake wa kiuchumi barani humo ikiwemo China. Kuenea harakati za kiuchuni za China, nchi ambayo inashika nafasi ya kwanza kwa kusafirisha bidhaa na kuwekeza barani Afrika, kumewatia kiwewe wakoloni wa zamani wa Ulaya na vilevile serikali ya Marekani. Pamoja na hayo, China imefanikiwa zaidi na kuwabwaga washindani wake barani Afrika kutokana na nchi hiyo ambayo haina historia ya ukoloni barani humo, kupeleka katika bara hilo bidhaa za bei nafuu na kutoa misaada ya fedha iliyojaa ukarimu na ubinadamu. Hali hiyo imeifanya China iwe nguvu kubwa yenye satwa na udhibiti kwa uchumi na mali barani humo.

Filihali, Marekani ina wasiwasi kwamba, uwepo huo wa kiuchumi wa China barani Afrika usije kubadilika na kuwa wa kisiasa na kiusalama na hivyo kuhatarisha ushawishi wa Washington. Ni kwa muktadha huo, ndio maana sambamba na kuanza safari ya Rex Tillerson, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani barani Afrika, serikali ya Washington imetangaza kuwa, itazipatia msaada wa dola nusu bilioni nchi za Kiafrika zilizoko katika hatari ya kukumbwa na mgogoro wa chakula. Pamoja na hayo, weledi wa mambo wanasema kuwa, ni jambo lililo mbali hatua hiyo ya Marekani ikasaidia kuirejesha nchi hiyo katika nafasi yake ya hapo kabla ya kisiasa na kiuchumi barani Afrika.

Tags

Mar 08, 2018 07:20 UTC
Maoni